Somalia
Viongozi wa upinzani nchini Somalia na majimbo ya mkoa wa Jubbaland na Puntland, pamoja na baraza la seneti la nchi hiyo, wamepinga uamuzi wa bunge la nchi hiyo kuongeza muda wa urais kwa miaka miwili.
Bunge la Somalia Jumatatu lilimwongezea muda Rais Mohamed Abdullahi Farmajo kuwa madarakani kwa miaka miwili huku serikali ya jimbo la Jubbaland limesema hatua ya bunge limekuwa kikwazo kwa kujenga upya utawala wa nchi hiyo.
Naibu Spika wa Kwanza wa seneti ya Somalia Abshir Ahmed alihoji nguvu ya Bunge dogo kuchukua uamuzi huo bila ya idhini ya seneti.
Pia kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Waziri Mkuu wa zamani wa Somalia Hassan Ali Khaire alisema rais “atawajibika tu kwa kile kinachotokea leo au kitakachotokea baadaye”.
Rais Farmajo alisifu uamuzi huo na kuwataka watu wa Somalia kutumia fursa hiyo na kushiriki katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.