29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani India ‘uchochoro’ kwa chama tawala

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

KWA wafuatiliaji wa siasa za barani Asia, hiki ni kipindi kizuri kwao kutokana na tambo zinazoendelea katika mikutano ya kampeni za wagombea wa nafasi mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa India, unaotarajiwa kufanyika Aprili 11, mwaka huu.

Ukweli ni kwamba uhondo ni katika kiti cha Waziri Mkuu, ambapo Narendra Modi wa Chama cha Bharatiya Janata (BJP), anayeshikilia wadhifa huo kwa sasa, amejitosa kuwania tena, kwa maana ya kurejea madarakani.

Je, ni rahisi kiasi gani kwa Modi, aliyeingia ofisini mwaka 2014, kuiongoza tena India mbele ya Congress, kinachoongozwa na Rahul Gandhi, mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Rajiv Gandhi? 

Rahul, aliyezaliwa Juni 19, 1970, ni mtaalamu wa masuala ya uchumi, akisomea Marekani na kufanya kazi London, Uingereza, kabla ya kurejea Mumbai mwaka 2002.

Awali hakuonekana kuvutiwa na siasa, badala yake muda wake mwingi aliutumia katika michuano ya kriketi, mchezo ambao mara nyingi amekuwa akijiweka karibu nao.

Jina lake katika ulingo wa siasa liliingia rasmi mwaka 2004, alipojitosa katika Uchaguzi Mkuu na kushinda kiti cha ubunge katika Jimbo la Amethi, ambalo awali baba yake alikuwa akilishikilia.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa hawaoni uwezekano wa Rahul kumzuia Modi na hiyo ni kutokana na upinzani dhaifu uliopo kuelekea Uchaguzi Mkuu huo unaotarajiwa kumalizika Mei 19, mwaka huu.

Ni kweli kama ilivyo katika mataifa mengi barani Afrika, changamoto kubwa inayoikabili India kwa sasa ni idadi kubwa ya vijana wasio na ajira. Ni moja kati ya ahadi ya Modi alipoingia madarakani miaka minne iliyopita, kwamba angehakikisha analimaliza tatizo hilo.

Takwimu zinaihukumu Serikali ya Modi, kwani iko wazi kuwa licha ya kwamba zaidi ya nusu ya wananchi wa India wana umri wa chini ya miaka 25, bado wengi wao hawana kazi.

Wengi wanakumbuka kuwa wakati wa kampeni zake za kusaka nafasi ya kuingia madarakani mwaka 2014, alisema: “Nchi hii… ina mtaji mkubwa wa vijana, lakini inahaha kusaka ajira, hali gani hii?”

Bahati mbaya kwake ni kwamba kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hali imekuwa mbaya zaidi, kwa mujibu wa Kituo cha Kusimamia Uchumi wa India (CMIE).

Kiwango cha wasio na ajira kimepanda kwa asilimia 6.1 kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2018, likiwa ni ongezeko kubwa zaidi kwa kipindi cha miaka 45 iliyopita.

Takwimu za CMIE ziliongeza kuwa, hali ni mbaya zaidi kwa vijana wa kijijini, kwani kiwango cha wasio na ajira kimepanda na kufikia asilimia 17.4.

Huku vijana wasomi wakigoma kabisa kufanya kazi zisizoendana na elimu zao, Serikali imekuwa ikinyooshewa kidole kwa kushindwa kuwa na sera makini, hivyo kupoteza mvuto kwa sekta ya kilimo.

Zaidi ya hali aliyoikuta, idadi ya vijana wanaotafuta kazi kwa bidii imeshuka kwa kasi, ikimaanisha kuwa wengi wao wameshakata tamaa.

Pia, bado wananchi wa India hawafurahishwi na hali ya usalama, hasa kutokana na uhasama uliopo kati ya nchi yao na Pakistan. Kitendo cha Bunge la India kushambuliwa mwezi uliopita kimewashitua, wasiamini kuwa wako salama ikiwa eneo hilo nyeti linaweza kuvamiwa.

Hofu ya wananchi wa India ni kwamba Serikali ya Modi imeshindwa kuweka mikakati ya kumaliza mgogoro wao wa muda mrefu na Pakistan. 

Licha ya kauli ya hivi karibuni ya rafiki mkubwa wa Modi, Amit Shah, kudai kuwa Serikali ya India imeshaua zaidi ya magaidi 250, wananchi wa India wanaamini hizo ni propaganda za kurejea madarakani tu.

Mmoja kati ya wakosoaji hao ni mpinzani wake mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Raul, ambaye alihoji: “Takwimu hizo zinatoka wapi?”

Licha ya changamoto nyingi alizonazo Modi, bado wachambuzi wa siasa za nchi hiyo hawaoni wapinzani watakavyoweza kumng’oa kiongozi huyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, BJP kimeonekana kuwa na nguvu kubwa ya kuuzima upinzani, jambo linaloonekana hata kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Awali, Chama cha Congress kinachoongozwa na Rahul (49) kilipewa nafasi kubwa ya kumng’oa Modi, lakini wachambuzi hawaamini kuwa hilo linaweza kutokea hata kwa bahati mbaya.

Imani ya wachambuzi inatokana na ukweli kwamba ana uhusiano mkubwa na Serikali, kama ambavyo hutokea kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani Afrika.

Kwa Raul kuwa mtoto wa aliyewahi kuwa waziri mkuu, Rajiv, wengi kati ya wachambuzi waliouzungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wameonyesha wasiwasi mkubwa juu ya upinzani wa kweli wa kuking’oa chama tawala, BJP.

Katika hilo la uhusiano wake na Serikali ya India, wachambuzi hawajasahau kuwa mwanasiasa huyo ni mjukuu wa Indira, mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya uongozi katika historia ya siasa za India.

Aidha, wapo wanaoamini kwamba, kwa kuwa babu yake, Jawaharlal Nehru, ndiye Waziri Mkuu wa kwanza India, si rahisi kumtenganisha Raul na maslahi ya Serikali. Hivyo basi, kuwa mpinzani ni sehemu ya ‘maigizo ya siasa’.

Je, vipi kuhusu kashfa zilizowahi kuibuliwa dhidi yake? Bila shaka zinaweza kumchafua. Haijasahaulika kuwa familia yake ilishawahi kubainika kuficha mabilioni ya fedha katika akaunti ya siri ya Benki Kuu ya Uswisi. 

Makandokando ya Raul yanahusisha pia skendo yake kubaka, ingawa mwishowe alidaiwa kusingiziwa kosa hilo, hivyo mahakama kumtaka mwanamke aliyeshitaki kulipa faini.

Awali, ilisemekana kuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa Chama cha Samajwadi, Kishore Samrite, alisema ni kweli kabisa kuwa Raul alimfanyia unyama huo mwishoni mwa mwaka 2006.

Hata wakati kesi hiyo ikiwa mahakamani, aliyewahi kuwa kiongozi wa upinzani bungeni, Oommen Chandy, alisema: “Kuna matukio mengi ya viongozi wa ngazi za juu wa Congress kuwadharau wanawake.” 

Ukiacha hilo, kuonyesha ni kwa kiasi gani upinzani nchini India umekosa nguvu mbele ya Chama tawala, BJP, Uchaguzi uliopita wa mwaka 2014 ulikishuhudia Congress kikiambulia viti 44 pekee kati ya 545 vya ubunge.

Wachambuzi wanaamini changamoto kubwa inayowakabili wapinzani ni kujikita zaidi katika kumshambulia Modi, badala ya kuelekeza nguvu zao katika kuwasilisha kwa wananchi mipango yao juu ya shida zinazowakabili wananchi wa India.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles