Na Kulwa Mzee, Dar es SalaamÂ
Upelelezi wa kesi ya aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka 43 yakiwamo kumiliki mali zisizo na maelezo, kughushi na kutakatisha fedha umekamilika.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Machi 20 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.
Wakili wa Serikali, Vitalis Peter amedai mahakamani kwamba kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelekezi umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kesi kutajwa.
Mahakama ilikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 4, mwaka huu kwa ajili ya kesi kutajwa na Aprili 10 mwaka huu washtakiwa watasomewa maelezo ya awali dhidi ya mashtaka yanayowakabili.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gugai, George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera ambao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kusomewa mashtaka yanayowakabili na Wakili wa Serikali Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Katika hati ya mashtaka Gugai anadaiwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015 akiwa Ofisa wa Umma aliyeajiriwa na Takukuru anamiliki mali yenye thamani ya Sh 3,634,961,105.02 ambayo haiendani na kipato chake cha sasa na cha nyuma ambacho ni 852,183,160.