29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YATOA ELIMU YA KODI KWA MAOFISA HABARI

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), hivi karibuni imekutana na maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini na kuwapa elimu ya masuala mbalimbali ya kodi hasa umuhimu wa kulipa kodi.

Mkutano huo ulifanyika jijini Arusha wakati wa kikao kazi kilichohusisha maofisa hao ambao TRA imewataka kuwa mabalozi wazuri katika sehemu zao za kazi na katika jamii wanazoishi kwa kuwaelimisha wananchi masuala mbalimbali yanayohusu  kodi.

Huo ni mwendelezo wa mikakati mbalimbali ambayo mamlaka hiyo imejiwekea ya kukutana na wadau wa kodi ili kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi.

Kwa mujibu wa TRA, Serikali ya Awamu ya Tano imewawezesha kufanya kazi ya ukusanyaji wa mapato kwa mafanikio, ikiwa ni pamoja na watu kuitikia wito wa kulipa kodi kwa hiyari.

Aidha, kutokana na mikakati mbalimbali iliyojiwekea ili kuhakikisha inafanikisha malengo yake hasa katika suala la ukusanyaji wa mapato, TRA imekuwa na mafanikio ya kuweza kukusanya zaidi ya Sh trilioni moja kila mwezi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema TRA imeweka utaratibu wa kukutana na wadau wa kodi ili kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi ili waweze kuwa mabalozi katika maeneo yao wanayoishi, ikiwa ni pamoja na katika sehemu zao za kazi.

Anasema lengo la kukutana na maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini ni kuwafundisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi, lakini pia ni kutaka kuwajengea uwezo wa namna ya kutangaza shughuli za Serikali na kuhakikisha Idara na Vitengo vya Mawasiliano na Uhusiano serikalini vinaimarishwa ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwahudumia wananchi.

Anasema hadi sasa wameshakutana na wadau wa kodi kutoka serikalini pamoja na sekta binafsi na kuwafundisha masuala mbalimbali ya kodi, kwamba zoezi hilo ni mwendelezo ili elimu hiyo imfikie kila mwananchi.

Anasema pia wamejipanga kuhakikisha elimu ya kodi inaanzia ngazi ya chini katika shule za sekondari ili waweze kutengeneza walipakodi wazuri wa baadaye, ikiwa ni pamoja na kuandaa maofisa wa mamlaka ya mapato wa baadaye.

Kayombo anasema kupitia maofisa uhusiano, elimu ya kodi itawafikia watu wengi kutokana na ushirikiano mkubwa walionao katika kutoa habari sahihi kwa umma.

Anasema kila mtu anachokifanya ni sauti kwa mwenzake katika eneo analokuwepo hivyo baada ya mafunzo hayo, maofisa hao wataisaidia mamlaka kuelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kodi katika maeneo yao ya kazi na maeneo mengine.

Anasema maofisa uhusiano wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii pamoja na kuwasahihisha pale wanapokuwa na elimu isiyosahihi kuhusu masuala ya kodi na ukusanyaji wa mapato kwa ujumla.

Anaongeza kwamba, TRA inasimamia kodi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kodi ya Mapato na Kodi ya Ongezeko la Thamani ambayo kwa jina lingine ni kodi ya mlaji.

Kayombo aliwaeleza maofisa hao kuwa ili kuweza kufanikisha kukusanya kodi hizo, TRA inawasisitizia wananchi kudai risiti kila wanapofanya manunuzi kutoka kwa wafanyabiashara waliosajiliwa na VAT.

Anasema iwapo mwananchi hatadai risiti, anakuwa amevunja sheria na kwamba anastahili kuchukuliwa hatua lakini pia anakuwa amemnufaisha mfanyabiashara huku akiikosesha Serikali mapato yake.

Anaongeza kuwa kwa kudai risiti kila baada ya manunuzi, kunaepusha udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kuficha mauzo halisi ambayo yanatumiwa na TRA kama sehemu mojawapo ya kukadiria kodi za wafanyabiashara hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles