24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

UPANUZI BANDARI YA MTWARA, DAR WAIVA

Na Joseph Lino


Bandari ya Mtwara ni miongoni mwa bandari zenye nafasi kubwa ya kuongeza uwezo wake kufuatana na maendeleo yanayofanyika huko na ukuaji wa shughuli za uchumi.

Kwa sasa bandari hiyo haitumiki kikamilifu kwa kukosa miundombinu ya uhakika na hivyo kuwa ni ‘bandari ya korosho’ inayofanya kazi kwa miezi mitatu kwa mwaka, hali ambayo inabidi ibadilike katika  enzi hizi za uchumi wa viwanda na ujaji wa gesi asilia.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alisema hayo alipofanya ziara katika Bandari ya Mtwara na kusema mchakato wa mradi wa kuboresha bandari hiyo unaendelea na kilichobakia ni kuhakiki na kutathmini ujenzi wa gati la mita 300 katika bandari hiyo.

Mradi huo ambao unakuja kipindi ambacho Mtwara imekuwa eneo lenye utajiri wa rasimali mbalimbali ikiwemo gesi na mafuta, uzalishaji wa saruji na shughuli za uchimbaji wa madini ya kinywe na urani na kilimo cha zao la biashara ya korosho na inategemewa kuwa itakuwa kiungo cha mzigo kutoka Mchuchuma na Liganga kama bandari mkakati ya madini kwa makaa ya mawe na chuma.

Waziri Mbarawa alisema Serikali inatarajia kuweka jiwe la msingi mwanzoni mwa Aprili mwaka huu.

“Nia ya Serikali ni kujenga gati nne katika bandari hiyo ambapo kwa kuanza itajenga gati moja,” alisema.

Kwa maelezo ya Waziri, awali ujenzi wa gati hiyo ulishindikana kufanyika kutokana na mkandarasi wa awali kudai malipo makubwa, lakini hakusema ni kiasi gani.

Prof. Mbarawa anasema ujenzi wa gati utakapomalizika, meli kubwa zenye urefu wa mita 300 zitaweza kutia nanga bandarini hapo.

Mradi wa ujenzi wa gati hilo utahusisha upanuzi wa mlango ambapo utachimbwa zaidi ili kurahisisha meli kubwa kuingia kwa urahisi.

Ujenzi wa gati katika Bandari ya Mtwara utaleta tija na ufanisi katika shughuli za maendeleo ya uchumi.

“Ujenzi wa gati hilo utawezesha meli za ukubwa wowote kutia nanga, jambo ambalo litasaidia mizigo mikubwa kufikishwa kwenye bandari hiyo,” alisema Mbarawa.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abilahi Salim, alisema ujenzi wa gati hilo utahusisha upanuzi wa mlango ambapo utachimbwa zaidi ili kurahisisha meli kubwa kuingia kwa urahisi.

Bandari ya Mtwara ilijengwa miaka ya 1950, ikiwa na uwezo kupokea mizigo tani 400,000 kwa  mwaka.

Aidha, Mbarawa wiki mbili zilizopita alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) vilevile itaipanua Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuongeza kina ili kuwezesha meli kubwa ambazo kwa sasa zinashindwa kutia nanga bandarini hapo kutokana na kina cha maji kuwa kifupi zifike.

Alisema Serikali inaendelea kuboresha bandari zake na zinalenga kuhakikisha kuwa bandari hizo zinawavutia wateja wengi.

“Naamini kwamba tukikamilisha miradi yote hii, bandari yetu itakuwa na uwezo wa kushindana na bandari nyingine yoyote katika Ukanda huu wa Mashariki mwa Afrika,” alieleza Prof. Mbarawa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Aloyce Matey, alisema Bandari ya Dar es salaam inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu na kuwa na kina kifupi cha maji cha mita 9 na ufinyu wa lango la kuingilia meli lenye upana wa mita 140 ambalo linaruhusu meli zenye urefu usiozidi mita 243 tu kuingia na meli kubwa zaidi kushindwa.

Bandari ya Dar es Salaam ilifanikiwa kupokea mizigo tani milioni 13.5 mwaka 2013 na tani milioni 14.4 mwaka 2014, kwa sasa ina uwezo wa kupokea zaidi ya tani milioni 18. Inatarajia kupokea tani milioni 28 ifikapo mwaka 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles