MANCHESTER, ENGLAND
UONGOZI wa timu ya Manchester United, umeweka wazi kuwa kocha wao Ole Gunnar Solskjaer ni mtu sahihi kwao ambaye anaweza kurudisha heshima ya kikosi hicho.
Wamedai wanamuamini kocha huyo japokuwa timu hiyo msimu huu imeanza kwa kusuasua. Katika msimamo wa Ligi England, Manchester United kwa sasa inashika nafasi ya nane baada ya kucheza michezo sita, wakishinda miwili, sare miwili na kufungwa miwili.
Jumla timu hiyo imepoteza michezo 10 kati ya 19 waliocheza kwenye michuano mbalimbali. Kipigo cha mwishoni mwa wiki kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya West Ham cha mabao 2-0, kiliwafanya mashabiki wa timu hiyo kuanza kuutaka uongozi timu hiyo kuuvunja mkataba wa kocha huyo.
Lakini United wanaamini kocha huyo bado anahitaji muda wa kutengeneza mifumo yake ambayo itaisaidia timu hiyo skufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali. Solskjaer alipewa jukumu la kuifundisha timu hiyo tangu Desemba mwaka jana akichukua mikoba ya kocha Jose Mourinho, lakini Solskjaer alikuwa kocha wa muda kwa kipindi cha miezi sita kabla ya kupewa mkataba wa moja kwa moja mwishoni mwa msimu uliopita.
Kutokana na hali hiyo, United wapo kwenye mipango ya kuweka mezani kiasi kingine cha fedha kwa ajili ya kumtaka aboreshe kikosi chake wakati wa uhamisho wa Januari mwakani.
Wakati wa usajili wa kiangazi mwaka huu, timu hiyo ilimpa Solskjaer kitita cha pauni milioni 150, ambazo ni zaidi ya bilioni 428 za Kitanzania kwa ajili ya usajili na alifanikiwa kuwanasa wachezaji kama vile beki wa kati kutoka Leicester City, Harry Maguire, Aaron Wan-Bissaka kutoka Crystal Palace na Dan James kutoka Swansea City, huku wakiwaacha Romelu Lukaku na Alexis Sanchez kuondoka na kujiunga na Inter Milan.