Bogota, Colombia
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi amehitimisha ziara yake ya wiki ya kutembelea nchi zilizoko Amerika ya Kusini na kuzishukuru nchi hizo kwa kazi kubwa ya kuhifadhi wakimbizi ambapo takwimu zinaonesha wamehifadhi zaidi ya robo ya wakimbizi wote duniani.
Takwimu za dunia zinaonesha kuna wakimbizi zaidi ya milioni 82 na asilimia 20 ya wakimbizi hao wamepewa hifadhi kwenye nchi za Panama,Colombia na Ecuador.  
Nchi hizo tatu zilizopo Amerika ya Kusini zinapokea mgeni maalum, Fillippo Grandi, Mkuu UNHCR ambaye amefika kuwashukuru na kujionea hali za wakimbizi. 
Akiwa Colombia, ameshuhudia utekelezaji wa ahadi ya kutoa vibali vya kuishi miaka 10 kwa wakimbizi wa Venezuela, programu iliyopitishwa rasmi mwezi Februari mwaka huu wa 2021. Pia alishiriki kwenye maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani. 
Shughuli zilizofanyika ni pamoja na uchoraji ili kuonesha vipaji vya wasanii, ambapo watu wazima na watoto wote waliimba na kufurahia siku hiyo.
Nchini Ecuador Grandi akiwa na mwenyeji wake Rais wa nchi hiyo na viongozi wengine wa ngazi za juu walishuhudia utekelezaji wa programu yakuwasaidia wafanyabiashara wahamiaji kutoka Venezuela ili waweze kujitegemea kiuchumi. 
Hapa pia alisherehekea siku ya wakimbizi kwa mtindo wa kisasa zaidi maana vijana wa Ecuador walimshirikisha kwenye kurekodi video kwa mitindo inayotamba kwenye mtandao wa Tiktok.
Kabla ya Colombia na Ecuador, Grandi alitembelea Panama, ambako alishiriki katika Mkutano wa kimataifa wa wahisani wa wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela.  
Alishuhudia nguvu ya vijana kujenga jamii wenye ari ya kufikia maendeleo yao. Zaidi ya wananchi wa Venezuela Milioni 5.6 wameikimbia nchi yao na kuomba hifadhi katika mataifa jirani.