Chuo cha St. John chazindua kitabu cha kumsaidia mwalimu kufundisha

0
327

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Chuo cha St. John cha Mkoani Dodoma kimezindua kitabu ambacho kitamsaidia mwalimu kutumia lugha rahisi, inayoeleweka iliyojaa mifano rahisi, picha na vielelezo kuhakikisha mwanafunzi anaelewa dhana ambayo inafundishwa.

Akizungumza Jumatano June 23, 2021,wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho kinachoitwa Language Sapportive Pedagogy: Theory, Implementation and Application, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John cha jijini hapa, Dk. Shadidu Ndossa amesema moja ya changamoto kubwa ambayo ipo katika ufundishaji ni namna ya kufundisha ili mwanafunzi aweze kuelewa kwa  lugha rahisi,inayoeleweka iliyojaa mifano rahisi, picha na vielelezo.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wanafunzi na walimu wa shule za Sekondari Kikuyu, Hazina, Welaa, Dodoma na Mkonze za jijini Dodoma.

Dk. Ndossa amesema kutokana ufundishaji kuwa ni changamoto walipata mradi wa Language Saporting Teaching and Text Book (LSTT) ambao ulikuwa na lengo la kumsaidia mwalimu kuweza kufundisha kwa lugha ya kueleweka.

Amesema kwa kupitia mradi huo wameweza kutunga vitabu vitatu vya Chemisty, Biology na Hisabati ambavyo vimekuwa msaada kwa wanafunzi na walimu.

Amesema mradi huo kwa sasa unaelekea mwishoni na walimu nane kutoka katika mradi waliweza kuandika kitabu kutokana na kushiriki katika mradi huo.

“Ni mradi ambao unahimiza mwalimu kutumia lugha au kuona lugha  ni sehemu muhimu kuhakikisha wanafunzi wanaelewa hasa katika masomo ya Sayansi. Kwa mfano mimi katika Chapter ambayo nimeiandika kama miongoni mwa waandishi niliandika kuelezea vile vitabu ni namna gani.

“Vimesaidia kumuunganisha mwalimu,mwanafunzi pamoja na vitabu kwa sababu kumekuwa na changamoto vitabu vinatumia lugha ngumu ikiwa ni pamoja na mifano ambayo haipo katika mazingira ya wanafunzi na tunatumia maneno magumu na sentensi ngumu.

“Kwa hiyo mradi wetu huu pamoja na mambo mengine unahimiza mwalimu kutumia lugha rahisi inayoeleweka na iliyojaa mifano rahisi,lugha iliyojaa picha na vielelezo kuhakikisha mwanafunzi anaelewa dhana ambayo inafundishwa,”amesema Dkt.Ndossa ambaye ni sehemu ya wahariri wa kitabu hicho.

Kwa upande, Kamishna wa Elimu, Kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Lyabwene Mtahabwa, amesema naamini watakaotumia kitabu hicho wataweza kuwa na njia bora ya kuwasilisha darasani.

“Na nimesema unapokuwa na uwezo wa lugha ya kufundishia unakuwa na raha nafsini kwako unakuwa na ujasiri na uwezo wa kuwasilisha kile ambacho umekiandaa kwa watoto kwa ufasaha zaidi lakini kinyume chake kama huna uwezo unakuwa unaogopa utafundishaje na kujibu maswali,”amesema ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

Pia, amewaomba wadau wa elimu kuiga mfano wa Chuo cha St. John katika kutafuta uvumbuzi wa changamoto ambazo zipo katika sekta ya elimu.

“Nikishukuru sana Chuo Kikuu cha St. John kwa kuona changamoto hii,lugha ya kufundishia ni muhimu kwa kitabu hichi naamini watakachokitumia kitawasaidia.Mimi nasema naomba wadau wengine na vyuo  viige mfano wa St John vieendelee kutafakari changamoto ambazo zipo na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi,”amesema.

Vilevile, amesema harakati zinaendelea katika kuboresha mitaala ya elimu kuhakikisha elimu ya Tanzania inaakisi maisha halisi ya Mtanzania.

“Zipo harakati zinaendelea kuboresha mitaala na pia iweze kuakisi hali halisi mchakato wa wadau umeanza na tutakuwa na kikao lengo kuhakikisha elimu yetu inaakisi maisha  halisi ya mtanzania kitaifa na kikanda kuhakikisha  Nchi yetu inasonga mbele,”amesema

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, Dk. Zawadi Richard amesema mradi wa Language Saporting Teaching and Text Book umemsaidia kuweza kuwasaidia walimu  waliopo katika shule za Sekondari na hata walimu wenzake ambao wanaotarajiwa kuwa walimu kujua mbinu za kufundishia.

“Suala la lugha  ya kufundishia imekuwa ni tatizo kubwa maana Kiingereza ni lugha  yetu ya tatu ama ya pili kwa watanzania lakini jinsi tunavyoendelea kutumia Kiingereza wanafunzi wetu tunaona wanazidi kupata shida.

“Kwa hiyo kupitia Programu hii tumeweza kuwasaidia walimu kwani wameweza kuwafundisha wanafunzi  kwa wepesi  hii inasaidia wanafunzi kuweza kuimporove kuelewa masomo yao na zaidia walimu waendeleee kujifunza kuwafundisha wanafunzi waelewe,”amesema

Naye, Mkuu wa Idara ya Somo la Kiingeraza kutoka Shule ya Dodoma Sekondari, Gerald Tibaigana  amesema umefika wakati wa kutunga kutunga vitabu kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.

“Na nishauri isiishie katika maeneo ya mijini pia ifike kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum tusiishie kwa wanafunzi ambao wanaweza kuona na kusikia basi tuwafikie hata ambao hawezi kusikia wasioona ili tuweze kufanikisha jambo hili,”amesema.

Amesema kupitia  vitabu vilivyotungwa ufaulu umeweza kuongezeka kwani awali kulikuwa na changamoto katika ufundishaji kwani wanafunzi wengi walikuwa hawaelewi.

“Nimefarijika sana kuona hili suala ambalo nililitilia mkazo kwakweli kabla ya hapo tulikuwa tunakutana na changamoto kubwa kwa mfano ufundishaji wa somo la Kiingereza ni mgumu sana  lakini sasa imetusaidia kuweza kuwasiliana.Tumefanikiwa kwani hata ufaulu umeongezeka na pia hichi kitabu kitaendelea kutusaidia,”amesema Mwalimu huyo.

Kwa upande wake,mwanafunzi wa shule ya Dodoma Sekondari,Vannesa Mwaihojo alikishukuru chuo cha St John kwa walimu wake kuweza kutunga kitabu hicho ambapo alidai kwa kutumia kitabu hicho kitaenda kuwasaidia  kujua lugha inavyoweza kutumika na kutusaidia kuweza kufaulu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here