Na CHRISTIAN BWAYA
WATU wengi huwa tunadhani kuwa kuna mtu mahali anaweza kutufanya tukawa watu wenye furaha. Mambo yanapokwenda kinyume na matarajio yetu, tunawalaumu watu tunaoamini ndio hasa waliosababisha tukakosa furaha. Pengine na wewe una mawazo kama hayo. Umeweka matumaini yako kwa ndugu, jamaa na marafiki unaoamini wanaweza kukuletea furaha.
Uzoefu, hata hivyo unaonesha kuwa mara nyingi matumaini haya tunayoyaweka kwa watu huyeyuka. Tuliofikiri watakuwa sababu ya furaha yetu wanageuka kuwa mwiba. Kwa kuwa tunafikiri wao ndio waliopaswa kuwa sababu ya furaha yetu, tunakata tamaa na kujawa na huzuni.
Pia, mara nyingi huwa tunafikiri vitu fulani vikitokea maishani basi tutakuwa  watu wenye furaha. Tunadhani, kwa mfano, tukiweza kutekeleza mipango fulani tuliyojiwekea katika kipindi fulani, basi tutakuwa watu wenye furaha. Lakini, uzoefu unaonesha kuwa furaha hiyo inayoletwa na kutimia kwa mipango fulani, hudumu kwa kipindi kifupi na kupotea. Furaha hiyo inapopotea, tunatafuta namna nyingine ya kuitafuta furaha.
Maana yake ni kwamba furaha haiwezi kuletwa na watu wala matukio mazuri yanayotupata. Kadhalika, furaha hiyo haiondolewi na changamoto tunazokutana nazo wala aina ya watu tunaokutana nao. Katika makala haya tunaangalia mambo kadhaa yanayoweza kukusaidia kuwa mtu mwenye furaha na kujiwekea mazingira ya kuwa mtu mwenye furaha kwa kubadili mawazo yako.
Jambo la kwanza, jifunze kuulisha ufahamu mambo yanayokujenga. Badala ya kutumia muda mwingi kusoma, kusikiliza, kuzungumza, kuangalia habari zinazosikitisha na kuumiza moyo, badili mazoea. Tangu unapoamka, shibisha ufahamu wako na habari zinazoinua moyo. Usisubiri watu wengine wakutie moyo. Jiinue moyo mwenyewe kwa kusoma mambo chanya, kusikia mambo yanayojenga na kutafakari mambo yanayokuinua. Kadiri unavyojenga mazoea haya, ufahamu wako utajaa habari njema na huo utakuwa mwanzo wa kuwa na furaha.
Upo ushahidi kwamba watu wengi hukata tamaa kwa sababu wanatumia muda mwingi kuulisha ufahamu wao mambo yanayokatisha tamaa. Watu hawa wanasikiliza watu wanaokatisha tamaa, wanafuatilia mambo yanayokatisha tamaa na hivyo ufahamu wao huwaandaa kukata tamaa. Badili chakula unachokipeleka kwenye ufahamu wako.
Inawezekana wewe ni miongoni mwa watu wanaoamini haiwezekani. Mawazo yako muda wote yanakutuma kwamba hutaweza. Unapofikiri mambo unayotaka kuyafanya, unajiaminisha pasi na shaka kwamba unajaribu tu lakini haiwezekani. Mara nyingi sababu ni mazingira uliyokulia. Inawezekana ulikejeliwa na kudhihakiwa kuwa huna unachoweza. Matokeo yako yamekubali uongo kwamba huwezi na huachi kujifikiria kama mtu duni na asiyejiweza kitu.
Hakuna sababu ya kuendelea kufikiria hivyo. Hupati faida yoyote kwa kujiona huwezi. Anza kujiona ni mtu wa maana, muhimu na anayetegemewa na watu. Tembea kifua mbele kwamba unaweza. Jisemee maneno ya kukuinua kwamba unaweza. Badili ile sauti uliyozoea kuisikia ikikunong’oneza kuwa huwezi, ikatae. Jisemee unaweza. Furaha yako itarejea.
Sambamba na hilo, unahitaji kujenga tabia ya kutarajia mambo mema hata kama huna uhakika yatatokea. Fahamu zetu, kwa kawaida, zimezoea kututarajisha mambo hasi. Inashangaza mara nyingi tunajikuta tunatarajia kuwa mambo mabaya yatatokea hata katika mazingira ambayo hatuna ushahidi wowote. Kwa mfano, unaweza kuwa unaandaa ripoti ya kupeleka kwa wakubwa wako wa kazi, lakini unafikiria namna watakavyoipinga ripoti hiyo. Kwanini usitarajie kuwa jambo jema litatokea badala ya kufikiria usichotaka kitokee? Jenga matarajio chanya kwa yale unayoyapanga. Tegemea mambo mazuri yatatokea.
Pia kuna tatizo la kufikiria mabaya yaliyowahi kutukuta. Unapofikiria mambo yanayokukatisha tamaa, mara nyingi, utajiumiza wakati hakuna unachoweza kukibadili kwa kuendelea kulea mawazo kama hayo. Ikiwa umewahi kushindwa jambo fulani ulilowahi kulipania hiyo haimaanishi utaendelea kushindwa milele. Hakuna sababu ya kuendelea kuamini fikra duni kwamba kwa sababu mabaya yalishatokea basi lazima yaendelee kutokea.
Pia, kuna tatizo la kujihesabia hatia. Wakati mwingine tunajiandikia hatia kwa makosa ambayo wakati mwingine ni watu wengine wameyafanya. Kujitesa kwa mambo yasiyo ya kwako binafsi na kujihesabia hatia ni kuifukuza furaha yako mwenyewe. Badili mtazamo wako na anza kuyachukulia makosa yoyote uliyowahi kuyafanya zamani kama sehemu ya maisha.
Lolote baya lililowahi kukupata huko nyuma haliwezi kuwa msingi wa utambulisho wako. Ni wakati wa kufuta historia ya mabaya yaliyokufundisha kujisikia vibaya. Itazame leo badala ya jana na kesho. Ifurahie leo utapate nguvu za kuiona kesho. Ukifikia hapo furaha yako haitategemea aina ya watu wanaokuzunguka wala matukio yanayokutokea bali imani thabiti inayoishi ndani yako kwamba furaha iko ndani ya uwezo wako mwenyewe.