Na ATHUMANI MOHAMED
UNAPOTAKA kufanikiwa katika maisha inabidi uhakikishe unatumia kila fursa inayokujia mbele yako kama chachu ya kukusogeza kwenye mafanikio.
Teknolojia ya mawasiliano imekuja na faida na hasara, lakini zaidi ukitumika vizuri husaidia zaidi kuliko kuharibu. Maana yake ni kwamba, ikiwa mtu atakuwa makini na teknolojia ya mawasiliano anaweza kutengeneza fedha nyingi.
Hebu jiulize; hii mitandao ya kijamii inakusaidia nini? Je, kuna cha zaidi unakipata nje ya mawasiliano ya kawaida? Tatizo ni kwamba kuna watu wanatumia mitandao vibaya.
Kutwa, kucha yeye na mtandao akipiga soga za hapa na pale. Siyo sawa hata kidogo. Ni vigumu kufanikiwa kimaisha ukiwa unapoteza muda wako.
UNAITUMIAJE SIMU YAKO?
Wakati siku zikiinza kuingia kwa kasi kipindi kile cha mwishoni mwa miaka ya ‘90 na mwanzoni mwa mwaka 2000, ilikuwa kununua simu ni anasa.
Ni kweli, maana kwanza wakati ule matumizi ya simu hayakuwa makubwa sana, lakini gharama zake zilikuwa kubwa. Mfano gharama ya kupiga simu ilitozwa kwa dakika nzima.
Hii inamaana kuwa, kama mtu amepiga simu na kuongea na mtu kwa sekunde tisa basi atalipia dakika nzima.
Kuandika ujumbe wa simu, uligharimu hadi Tsh. 120 kwa meseji moja tu na ukumbuke kuwa vocha (muda wa maongezi) zilinunuliwa kwa kulinganisha na Dola ya Marekani.
Kwa mfano unanunua vocha ya Dola 5, kwa hesabu za sasa ni kama umelipia Tsh. 11,000. Hata katika matumizi, pia watumiaji walitozwa kwa dola.
Kwa kifupi kutumia simu ilikuwa anasa, maana gharama zilikuwa kubwa sana, lakini ukweli ni kwamba kwa sasa hali imekuwa mbaya zaidi.
Gharama ni kubwa maradufu kuliko hata wakati ule. Katika kipindi hiki cha simu za smart, kuweka bando la internet ni gharama tofauti na kupiga au kutumiana ujumbe mfupi.
Hii inamaanisa kwamba kukaa sana kwenye makundi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook, Twitter na mingine mingi utatumia fedha nyingi.
TAFUTA FURSA
Unatakiwa uwe mjanja. Kwa namna mambo yalivyo huwezi kukwepa mitandao ya kijamii kabisa. Utajikuta umeungwa kwenye makundi ya familia, marafiki, kazini, harusini, kanisani nk.
Wakati mwingine inawezekana upo kwenye makundi mazuri, muhimu ambayo kutokana na umuhimu wake unashindwa kujitoa, lakini hilo lisikuvunje moyo, tumia makundi hayo kama mtaji kwako.
Soma kwa makini mambo mbalimbali yanayoandikwa na kujadiliwa katika makundi hayo. Unaweza kukutana na mjadala wenye tatizo kubwa kwa jamii, ukauchukua na kuufanya mradi. Kwanini nasema mradi?
Ni kwa sababu utatafuta majibu ya changamoto hiyo ambayo sasa itakupa fedha. Acha kuwa mtu wa kupiga soga, zingatia zaidi yale ya muhimu na yenye tija kwako.
Utajikuta wenzako wapo busy wakichati wakati wewe ukitengeneza maisha. Acha kufanya mambo kwa mazoea. Mitandao ya kijamii siyo mibaya. Ni suala la kutuliza akili na kutumia kama fursa ya mafanikio kwako.
Simu ya smart inaweza kuwa na faida zaidi ya kuchati kama unavyofanya sasa. Fikiri tofauti na uchukue hatua.