LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Arsenal, Unai Emery, anaamini amepata nafasi sahihi ya kumtumia kiungo wa timu hiyo, Mesut Ozil, katika kikosi chake cha kwanza wakati kitakaposhuka dimbani leo kuvaana na Everton katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid, alikuwa katika wakati mgumu kuhakikisha anamshawishi kocha huyo ambaye amerithi mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger.
Majeruhi pia yalichangia Ozil kuonekana mzigo katika kikosi cha Emery ambaye kwa sasa baada ya michezo minne ameanza kumwamini.
Mchezo wa mwisho uliochezwa Jumatatu iliyopita dhidi ya Newcastle United ambao Arsenal ilishinda mabao 2-0, Ozil alikuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kikosi cha Emery kinaweza kuipiku Tottenham nafasi ya pili iwapo itaifunga Everton leo wakati Ozil akitarajia kuanza kikosi cha kwanza.
Akieleza sababu ya kumtumia kiungo huyo katika kikosi cha kwanza, Emery alisema inatokana na kuhitaji kitu cha tofauti katika kikosi chake.
“Kuna wakati tunahitaji kitu cha tofauti katika kikosi, wakati mwingine anakosekana kutokana na kuwa majeruhi na sasa tunamtumia kwa sababu tunamhitaji.
“Ni sawa, anafanya mazoezi kila siku, anaweza kucheza katika nafasi mbili kwenye mfumo tofauti ukiwamo 4-2-3-1 ambao ni sehemu inayomfanya afanye vizuri au mfumo wa 4-3-1-2 ambao anacheza kama kiungo mchezeshaji.
“Nafikiri tunaweza kumtumia katika mifumo hiyo akiwa kulia au kushoto, jambo la muhimu awe tayari kutusaidia na sasa yupo katika kiwango bora,” alisema Emery.