24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA SC NGOMA NZITO

NA THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya jana kulazimishwa suluhu na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa italazimika kupata ushindi wa aina yoyote dhidi ya Mazembe katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Aprili 13, Uwanja wa Mazembe jijini Lubumbashi, DRC.

Katika mchezo mwingine wa robo fainali, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikiwa nyumbani iliiadhibu Al Ahly mabao 5-0.

Dakika ya nne, Mazembe walifanya shambulizi, lakini mabeki wa Simba walijipanga imara na kuondosha mpira kwenye hatari.

Dakika ya tano, mwamuzi Mustapha Ghorbal alimwonyesha kadi ya njano mshambuliaji, Muleka kwa kujiangusha eneo la hatari la Simba. 

Dakika ya saba, Simba ilipata pigo baada ya beki wake wa kati, Pascal Wawa kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Jjuuko Murshid.

Dakika ya 13, John Bocco angeweza kuiandikia Simba bao la kuongoza, lakini mpira wake wa kichwa ulipaa juu ya lango la Mazembe.

Simba iliendelea kufanya mashambulizi, dakika ya 16, kiki ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyepokea pande  zuri la Jonas Mkude, mkwaju wake ulipaa juu ya lango la Mazembe.

Dakika ya 18, alionyeshwa kadi ya njano kwa kumwangusha Abdoulaye Sissoko wa TP Mazembe nje kidogo ya boksi.

Dakika ya 31, Meddie Kagere aligongesha mwamba wa pembeni wa Mazembe baada ya kuunganisha kwa ‘tik-tak’ krosi ya Zana Coulibaly.

Dakika ya 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa pasipo nyavu za pande zote kuguswa.

Kwa jumla kipindi cha kwanza Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na kutengeneza mashambulizi mengi kulinganisha na wageni wao, ambao walionekana walifanya mashambulio ya kushtukiza.

Kipindi cha pili Simba iliingia na mpango ule ule wa kushambulia kwa kasi, ingawa umakini mdogo wa wachezaji wake ulionekana kikwazo cha Wekundu hao kukosa mabao.

Ili kuongeza tija katika kikosi chake, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alifanya mabadiliko kwa kumtoa Clatous Chama na kumwingiza Emmanuel Okwi. 

Dakika ya 58, mwamuzi Ghorbal aliizawadia penalti Simba, baada ya beki wa Mazembe, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Kagere.

Penalti hiyo ilipigwa na Bocco, lakini alishindwa kuiandikia Simba bao baada ya mkwaju wake kupaa juu ya lango la Mazembe.

Dakika ya 63, Mkude alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Jackson Muleka wa Mazembe.

Dakika ya 64, Mazembe ilifanya mabadiliko, alitoka Sissoko Abdoulaye na kuingia Nathan Sinkala, kabla ya dakika ya 81 kufanya mabadiliko mengine, ambapo alitoka Tresor Mputu na kuingia Glody Likonza.

Dakika ya 84, mkwaju wa mpira wa adhabu wa Okwi ulipaa juu kidogo ya lango la Mazembe.

Mazembe ilipoteza nafasi nzuri mno dakika ya 89, baada ya kiki ya Likonza kugonga mwamba wa kulia na kutoka nje, akiwa amebaki yeye na kipa, baada ya kuwatoka mabeki wa Simba.

Hadi kipyenga cha kuashiria kumalizika kwa pambano hilo kinasikika matokeo yalikuwa 0-0.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles