Umoja wa Mataifa (UN) umetaka uchunguzi ufanyike juu ya kifo cha mwanaharakati aliyekuwa akiikosoa Serikali iliyoko madarakani chini ya Rais Mahmoud Abbas.
Mjumbe wa Amani wa UN kwa nchi za Mashariki ya Kati, Tor Wennesland, amesema leo Juni 24, 2021 kuwa; “Wahusika wanatakiwa kufikishwa mbele ya sheria,” amesema.
Nizar Banat, alikuwa akiunyooshea kidole utawala wa Rais Abbas, ikiwamo kumtaja kiongozi huyo kuwa ni fisadi na hivi karibuni alishikiliwa na vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa familia yake, Banat mwenye umri wa miaka 43 alitembezewa kichapo baada ya kukamatwa na polisi jijini Hebron.
Akisimuliwa kukamatwa kwake, Hussein Banat ambaye ni binamu yake Banat anasema waliamshwa na sauti za polisi walioingia ndani kwa kuvunja mlango na madirisha.
“Walimpiga kichwani kwa nondo walizotumia kufungua madirisha,” amesema Hussein (21).