Umoja wa Mataifa umesema jumla ya watu 56 wameuliwa huku 266 wakijeruhiwa katika muda wa siku sita nchini Libya ambako vikosi vya jeshi la Mashariki mwa Libya vinakabiliana na vikosi vitiifu kwa Serikali ya Tripoli.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa haikufafanua wengine waliofariki ni raia wa kawaida ama ni wanajeshi wanaoshiriki makabiliano hayo ambapo kiongozi wa kijeshi anayeongoza eneo la Mashariki mwa Libya Khalifa Haftar wiki iliyopita aliamrisha jeshi lake kwenda kuuteka mji wa Tripoli.
Jeshi hilo la taifa la Libya linaloongozwa na Haftar (LNA) hadi leo asubuhi lilikuwa limeshikilia vitongoji mbali mbali kilomita 11 kusini mwa mji mkuu Tripoli ambako vita vinaendelea na hadi sasa maelfu wamekimbia makaazi yao.
Mwanachama wa kamati ya mizozo katika manispaa ya Tripoli, Nasser Al Kario aliliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kwamba janga la binadamu linaweza kufika katika mji mkuu iwapo vita hivyo vitaendelea na kuingia ndani ya mji wa Tripoli ambapo kuna watu zaidi ya milioni mbili.
Al Kario alisema kamati yake haina rasilimali za kutosha kushughulikia ongezeko lisilotarajiwa la raia wasio na makaazi na iwapo vita hivyo havitositishwa basi wanatarajia maelfu ya watu kuachwa bila makao.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitaka vita hivyo kusitishwa ili kuepuka umwagikaji mkubwa wa damu mjini Tripoli huku akiwaambia wanahabari kwamba kuna wasiwasi mkuu sio tu kwa maisha ya watu wa Libya bali pia kwa wahamiaji na wakimbizi mjini Tripoli na raia wa kigeni na kwa hivyo wana kila sababu ya kutaka vita hivyo kusistishwa.
“Ni wakati wa kusitisha vita. uko muda wa kuweka chini silaha, ili kukomesha vita kuendelea na kuepuka maafa zaidi ambayo yatakuwa ni vita vya damu kumwagika. Ninafurahi shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi liliweza kuhamisha moja ya kambi ya wakimbizi. Ni wazi kabisa kwangu kwamba tunahitajika kuanza upya mazungumzo ya dhati ya kisiasa ila bila shaka hayo hayawezi kufanyika bila kusimamisha vita hivi kabisa,” alisema Guterres.