25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Umuhimu wa kulinda hisia za mtoto

Na CHRISTIAN BWAYA

WIKI iliyopita, msomaji mmoja ambaye hata hivyo, hakujitambulisha jina, aliniandikia ujumbe ufuatao: “Mimi katika maisha yangu sijawahi kuwa na furaha kutokana na malezi niliyolelewa na wazazi wangu kwani sijawahi kuona upendo kati yao na kwangu kama mtoto. Sasa naona unipe njia ambazo zinaweza kunifanya niweze kuishi maisha ya furaha.”

Mwingine, naamini baada ya kusoma makala ya wiki iliyopita iliyohusu wazazi kuingilia maamuzi ya watoto wao, aliniandikia:

“Mimi na baba yangu mzazi nikifanya jambo la maendeleo hataki ananiwekea fitna kama sio mtoto wake. Mambo mengi ananifanyia.”

Wasomaji hawa wanawakilisha mitazamo ya watoto wengi wanaojisikia kuwa wahanga wa malezi. Nimetumia neon ‘kujisikia’ kwa sababu inawezekana kabisa wazazi wao, kwa upande mwingine, wanaweza kushangazwa na madai hayo kwa sababu wanaamini wanawapenda. Hayo yanayoonekana kuwa ni makosa, kwao ni wajibu wa mzazi kwa mtoto.

Hata hivyo, ni vyema kuelewa kuwa matatizo mengi katika familia huanza pale wazazi tunapojaribu kupuuza hisia za watoto kwa sababu wanaamini hazina usahihi. Matokeo yake, majeraha ya hisia hizo huwa makubwa na yanaweza kuathiri uhusiano wa mzazi na mtoto kwa miaka mingi baadae. Tukitumia mifano ya wasomaji, tunaona kwamba hata katika mazingira ambayo kwa macho ya mzazi mtoto anakosea, bado hatuwezi kupuuza ukweli kwamba mtoto anajisikia vibaya.

Msomaji wa kwanza mathalani, anaamini hakupendwa na wazazi wake kwa sababu kama anavyoeleza mwenyewe, wazazi hawakuonesha mfano wa upendo kati yao. Huu unaweza kuwa ujumbe muhimu kwa wazazi. Je, maisha yako yanawafanya watoto wauelewe upendo? Je, unaishi maisha yanayoonesha mfano wa upendo kati yenu? Tuzingatie kuwa vile tunavyoishi, watoto hujifunza. Ikiwa tuna tabia ya kuzozana mbele yao, fahamu zao zinarekodi chuki, ugomvi na kutokuwapo kwa amani hata kama kwa maneno unawahakikishia kuwapenda.

Kwa upande wa watoto wanaojiona kuwa waathirika wa familia zisizo na upendo, ni vizuri kuelewa kuwa wakati mwingine wazazi wetu hawafanyi makusudi. Wakati mwingine, maisha waliyoishi ndiyo waliyoamini ni sahihi kwa sababu yalikuwa sehemu ya utamaduni. Lakini hata katika mazingira ambayo ni kweli walikosea, bado tunahitaji kuwasamehe kwa sababu hatujui mazingira yaliyowafanya wakaishi maisha hayo tunayoyakumbuka.

Wito wangu kwa msomaji wa kwanza ni kuwasamehe wazazi. Maisha yako hayategemei historia yako. Inawezekana ni kweli wazazi hawakukupenda. Inawezekana walisema maneno ya kukudhalilisha na ukayaamini na pengine ni kweli yameathiri namna unavyojitazama na kuwatazama watu wengine. Pamoja na hayo yote, bado unaweza kuanza upya kwa kujifunza kujipenda.

Hatua ya kwanza ni kusamehe. Hatua ya pili ni kuelewa kuwa furaha ni zao la yale unayoyaamini. Ukiamini kuna mtu mwingine ndiye anayewajibika kukuletea furaha, hutokaa uwe na furaha. Lazima uanze kubadili fikra na kuelewa kuwa wewe ndiye mwenye ufunguo wa furaha yako mwenyewe. Jenga urafiki na watu watakao kuambia maneno chanya. Jenga mazoea ya kutazama mambo kwa mtazamo chanya badala ya kujihurumia. Furaha yako itarejea.

Kwa msomaji wa pili, pengine huu ni ujumbe kwetu wazazi. Je, mzazi anaweza kumfitini mtoto? Mambo yapi tukiyafanya kwa watoto wetu wanaweza kuyatafsiri kama fitna kwao?

 

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles