Unapoingia kwenye uhusiano hakikisha mwenza wako amekomaa kifikra

0
1439

Na CHRISTIAN BWAYA

MITAFARUKU mingi inayosumbua ndoa ingeweza kuepukika kama wapenzi wasingepuuza dalili za hatari.  Mara nyingi dalili hizi huonekana mapema lakini mapenzi huwafanya wapendanao kuzipuuza wakiamini zitaondoka. Madhumuni ya mfululizo wa makala hizi ni kumsaidia kijana anayejiandaa kuingia kwenye uhusiano wa kudumu, aghalabu ndoa, kupata mwangaza wa mambo ya kushughulikia kabla hajala kiapo cha ndoa.

Wiki iliyopita tuliangazia masuala kadhaa yanayohusu uaminifu. Tulieleza kwamba haiwezekani kuwa na ndoa imara na mwenzako ikiwa mmoja wenu hana uaminifu. Sura ya kwanza ya uaminifu ni kuishi maisha yenye mipaka, kujua nini sipaswi kukifanya na kipi naweza kukifanya lakini kwenye mazingira fulani. Sura ya pili ya uaminifu ni uwezo wa kulinda urafiki katika mazingira yoyote. Tuliutazama uaminifu kama hali ya kutokuwa na wasiwasi kuwa mwenzako anaweza kukugeuka katika mazingira Fulani fulani. Tulihitimisha kuwa unapoona dalili za mtu kukosa uaminifu kabla ya ndoa, usipuuze.

Katika makala ya leo ningependa tutazame kidogo suala la ukomavu. Katika muktadha wa makala haya, ukomavu ni ule uwezo wa kujisimamia na kufanya uamuzi wako mwenyewe bila kutegemea zaidi nguvu kutoka nje. Sina maana ya kutokuhitaji ushauri kwa mtu yeyote bali kuwa na ule uwezo wa kutafakari ushauri unaoupata na kuufanyia kazi pale inapobidi.

Upande mwingine wa ukomavu ni ule uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza bila kuumiza hisia za wengine. Tunafahamu, ukitaka kujua kiwango cha utu uzima alichonacho mtu tunatazama namna anavyokabiliana na mabaya yasiyo tarajiwa. Ndio kusema, mbali na idadi ya miaka aliyokuwa nayo mtu, ukomavu wake huonekana pale anapoweza kumudu changamoto mbalimbali anazokutana nazo. Mtoto, shauri ya ubinafsi, huhamaki anapokutana na magumu na matokeo yake kuzalisha matatizo mengine. Lakini mtu aliyekomaa anao uwezo wa kushughulikia mambo magumu bila kuyakuza na kuyafanya yazalishe matatizo mengine.

Swali ni je, unawezaje kujua ukomavu wa mtu? Je, mtu anaweza kuwa na miaka 40 na bado akashindwa kuwa mtu mzima? Katika kujibu swali kama hili, nikupe kisa kimoja.

Idris, kijana wa miaka 33 amemuoa Shadya, mwanamke anayempenda sana. Miezi michache baada ya ndoa yao, Shadya analalamika kutokuwa na mawasiliano mazuri na mama mkwe wake ambaye ndiye mama wa Idris. Tangu akiwa kijana mdogo, Idris alikuwa na ndoto ya kuwa na mke atakayekuwa karibu na mama yake. Taarifa kuwa mke wake Shadya haelewani na mama yake zinamchanganya. Ingawa anampenda sana mke wake Shadya, Idris anaanza kupatwa na wasiwasi na tabia hiyo ya mke wake akiamini ana chuki binafsi na mama yake. Haraka haraka Idris anakwenda kwa mama yake kujaribu kuelewa kulikoni haelewani na mwali wake.

Maelezo ya mama yanaonesha namna gani Shadya ni tatizo jipya katika familia. Kichwa cha Idris kinabeba taarifa hizo kama zilivyo kwa imani kuwa mama hawezi kukosea. Hapo ndipo matatizo katika ndoa yanapoanza. Ufa mkubwa unajitokeza kati yake na mkewe. Kubwa ni imani kuwa Shadya si mtu mwema. Hata katika nyakati chache anapofanya maongezi na mkewe, Idris haonekani kuelewa kuwa Shadya naye kwa upande wake anaweza kuwa na hoja za msingi. Imani kuwa hakuna namna mama yake anaweza kuwa upande wa kukosea, inamfanya hata anapozungumza na mkewe awe kwenye upande wa kushutumu na kuonesha makosa.

Visa kama hivi vipo kwenye familia nyingi. Mke anakuwa haelewani na wakwe zake wakati mwingine kwa sababu zao binafsi lakini mume hayuko tayari kuvaa viatu vya mke wake. Idris ni mfano wa wanaume wengi wanaojaribu kutatua tatizo kwa kuzalisha tatizo. Badala ya kujenga daraja kati ya mama yake na mkewe bila kutengeneza mtafaruku zaidi, Idris anashughulikia malalamiko ya mke wake kwa kuzalisha mtafaruku mkubwa zaidi. Badala ya kutazama tatizo kwa picha pana, Idris anatumia macho ya mtu mmoja kufanya uamuzi.

Kwa upande mwingine, inavyoonekana, Idris anaamini kumpenda mama yake maana yake ni kutokuona dosari yoyote kwake. Ingawa kwa juu juu hili linaweza kutafsiriwa kama busara na utiifu kwa mama, ukweli ni kwamba mtazamo huu unaweza kumfanya Idris akawa kipofu wa hisia za mkewe zinazoweza kuwa sahihi pia.

Watu kama Idris huwa ‘hawaondoki nyumbani.’ Wanakuwa tayari kupuuza hisia za wake zao kwa minajili ya kulinda hisia za upande mmoja bila kujipa muda wa kufanya utafiti. Wanasahau kuwa ukomavu ni pamoja na kutokumpendelea mtu Fulani kwa gharama ya kumuumiza mwingine.

INAENDELEA

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here