Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
NI miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Freedom House ya nchini Marekani, inayojishughulisha na utetezi wa haki za msingi za watu.
Chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wanatekeleza mradi wa ‘Data Driven Advocacy’ (DDA), unaozijengea uwezo Asasi za kiraia ziweze kutengeneza takwimu na kuzitumia katika ushawishi na utetezi.
Ofisa Miradi Mwandamizi wa Freedom House, Daniel Lema anauzungumzia mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na taasisi hiyo akisema tayari wamefanya kazi katika maeneo kadhaa.
“Kwanza tunaangalia kama mradi ni suala la kufubaa au kufinyika kwa nafasi ya raia katika uendeshaji shughuli za Serikali.
“Kwa maana hiyo, tunazijengea uwezo asasi za kiraia kuwa sauti ya wananchi katika kutetea masuala ya utendaji kazi,” anasema Lema.
Analitaja jambo la pili linalotekelezwa na taasisi hiyo kuwa ni kuangalia unyanyasaji na ukatili kwa wanawake, watoto, ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo na watu wenye ulemavu.
Kupitia eneo hilo, wameainisha asasi za kiraia wanazofanya nazo kazi kuwa ni PINGO’S Forums na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF).
Jambo la tatu linalotekelezwa na mradi huo ni kuangalia ushiriki wa vyombo vya habari katika kutetea, kulinda haki na uhuru wa wananchi na kuwa wasemaji wa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Anasema kwa sasa, wigo wa kutembelea mitandao ya kijamii (Alternative Media), umepanuka na vyombo hivyo kujikuta vikifanya kazi pana zaidi ya kuhabarisha watu tofauti na vyombo vya habari vilivyozoeleka.
“Tulibaini eneo la Alternative Media halijaimarishwa kwenye mafunzo kwani ndani kuna waandishi wanahitaji kunolewa zaidi katika masuala ya kuwajengea uwelewa wa kufanya kazi na kufikisha habari kwa umma.”
Anasema baada ya kukamilika kwa miaka mitano ya mradi, wanatarajia kuona jamii endelevu yenye misingi ya haki za binadamu na watu inayoheshimiana na kutetewa.
Ikiwamo pia kuona weledi mkubwa wa ufanyaji kazi kwa asasi na wanahabari watakaoshiriki kwenye mradi huo.
“Tunataka kuona watu waliojengewa uwezo wamekuwa na uelewa wa kuchambua na kufanya mambo yatakayoleta mguso kwa jamii.
“Mradi huu unatarajia kuona matumzi ya takwimu yanakuwa muhimu zaidi katika kazi za utetezi. Tunataka kuzijengea uwezo asasi za kiraia namna ya kuziinua ili zijimarishe kwenye eneo hilo.
“Mwenye takwimu akizungumza watu humsikiliza kwa sababu amefanya kazi na kuwasilisha taarifa zilizofanyiwa utafiti na si porojo,” anasema Lema.
Zipo changamoto ambazo tayari katika kipindi cha kuelekea miaka miwili wamekutana nazo, ikiwamo kukosekana kwa mitandao makini yenye wanachama hai na wanaoiheshimu.
“Ipo inayojiita mitandao, lakini ukiiangalia kwa makini utabaini ni shirika. Ili uwe na sifa za kuwa mtandao lazima uwe na wanachama waliosambaa nchi nzima,” anasema Lema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mradi DDA, kupitia taasisi ya Freedom House, Rosemary Mwakitwange, anasema tayari wanaendelea kutoa mafunzo muhimu kwa wanahabari na watendaji wa asasi za kiraia.
“Tumeendesha mafunzo ya Usalama katika Teknolojia ya Dijitali kwa wanahabari wa vyombo vya habari mbadala na watendaji wa asasi za kiraia, mafunzo mengine yalitolewa mjini Morogoro yakilenga kuwajengea uwezo wanahabari wafahamu sheria na kujiweka katika mazingira salama,” anasema Mwakitwange.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa mradi wa DDA, Wakili Clarence Kipobota, anasema mradi wa DDA unafanya ushawishi na utetezi kwa lengo la kubadilisha jambo katika jamii kwa kutumia ushahidi wa takwimu au kitu kingine katika kukijengea hoja kwa jambo linalotetewa ili lilete mashiko.