Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Umoja wa Wanawake Viongozi Serikalini umetoa mashuka 400 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, vituo vya afya vya Makole na vya wilaya ya Kongwa na Chamwino na kile cha Mbagala Rangi tatu jijini Dar es Salaam ili yaweze kuwasaidia akina mama.
Mashukuka hayo yamekabidhiwa leo Jumosi Machi 16, 2024 jijini Dodoma na Katibu wa Umoja huo, Sakina Mwinyimkuu kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Grace Magembe ambaye naye alimkabidhi Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Baraka Mponda pamoja na Daktari Bingwa wa magonjwa ya kina Mama Dk. Enid Chiwanga.
Pia, Umoja huo ulitoa zawadi kwa madaktari na wauguzi wanaohudumia wodi za kina mama.
Naibu Katibu Mkuu Afya, Dk. Maghembe ameushukuru Umoja huo kwa kutoa mashuka hayo ambapo amesema yatakuwa msaada mkubwa kwa Serikali.
“Kule Mbagala Rangi tatu wale wanajua kujifungua na hapa (General) pia kuzuri kina mama wanajifungua wengi na wanajaza dunia kweli kweli,” amesema Dk. Maghembe ambaye naye ni mmoja wa wahusika katika umoja huo.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja huo, Sakina amesema huo ni mwezi wa wanamke hivyo wameamua kuadhimisha kwa kutoa mashuka 400 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na vituo vya afya, Makole, Kongwa, Chamwino na Mbagala Rangi tatu na kwamba tayari wametoa msaada kwa wanawake wa Magereza.
Sakina amesema malengo manne ya Umoja huo ni kuwajengea uwezo viongozi Wanawake kutoka katika Taasisi mbalimbali, kusaidia viongozi vijana ili kuwaandaa katika uongozi, kutoa fursa kwa wastaafu na kusaidia jamii.
Naye, Daktari Bingwa wa magonjwa ya kina Mama kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Chiwanga amesema walikuwa na mhitaji makubwa ya mashuka hivyo wanaushukuru Umoja huo kwani watapunguza changamoto hiyo.
Amesema Mama mmoja amekuwa akitumia zaidi ya mashuka nane hadi kujifungua.
Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya kina mama amesema wanaushukuru Umoja huo pamoja na Serikali ya awamu ya sita kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Peres Lukango amesema anatamani mwaka mzima uwe wa Wanawake kutokana na namna walivyojitoa kwa kuisaidia jamii.
“Tunafurahi mnajua tunahitaji kipi na kwa wakati upi tunafurahia uwepo wenu na kuijali jamii,”amesema Dk. Lukango.