Amina Omari -Tanga
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewashauri wanaume kutoogopa kufanya kipimo cha saratani ya tezi dume kwani kwa sasa kipimo kinachotumika ni cha damu.
Hayo aliyasema jana jijini Tanga, wakati wa uzinduzi wa kambi ya huduma ya afya ya magonjwa yasiyoambukiza iliyohusisha madaktari waliosoma nchini China.
Alisema kuwa kwa sasa kipimo hicho kimerahisishwa na kuwa ni kwa kutumia damu pekee unaweza kugundulika ugonjwa huo.
“Wanaume mlikuwa mnaogopa kwenda hospitali kupima tezi dume, hivyo niwaambie jitokezeni kwa wingi kwenye kambi hii kwani hatutumii kile kipimo mnachokihofia,” alisema Ummy.
Alisema kuwa magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni changamoto kubwa kutokana na kuathiriwa watu wengi nchini na sababu yake kuu ni mabadiliko ya mfumo wa maisha.
Ummy alisema uwepo wa kambi hiyo ya matibabu ya bure umekuwa ukisaidia kuhudumia wananchi wengi na hivyo kusaidia kuwapunguzia gharama za matibabu kwa kiasi kikubwa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, alisema kuwa kambi hiyo itakayodumu kwa siku tano, imelenga kutoa huduma za vipimo, matibabu na ushauri wa kiafya bure.
Nao wananchi waliojitokeza katika kupata huduma, waliiomba Serikali kuhakikisha wanasogeza huduma za uchunguzi wa saratani katika maeneo ya karibu.
Mmoja wa wananchi hao, Emmanuel Mgomba, alisema kuwa huduma hiyo itaweza kuwasaidia kubaini changamoto za magonjwa mapema na kupatiwa matibabu yanayostahiki kwa wakati.