KKKT yapongeza Serikali ujenzi wa miradi ya maendeleo

0
877

Elizabeth Kilindi -Njombe

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeipongeza Serikali kwa kuleta maendeleo katika miundombinu ya barabara, reli na anga, kuhimiza maendeleo ya viwanda ili kuwawezesha Watanzania kuuza bidhaa zilizoandaliwa, ikiwa ni pamoja na kutoa uhuru wa kuabudu.

Pongezi hizo zimetolewa jana mjini Njombe na Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Awamu ya Sita, Dk. George Fihavango, baada ya kuwekwa wakfu kuwa askofu wa dayosisi hiyo katika ibada takatifu iliyoongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Frederick Shoo.

Askofu Fihavango alisema Kanisa linaishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa dayosisi yake, hususani katika sekta ya afya.

“Dayosisi yangu ina ubia na Serikali wa kutoa huduma za afya kupitia Hospitali Teule ya Kilutheri Ilembula iliyopo Wanging’ombe ambapo kati ya watumishi 182 waliopo, Serikali inalipa mishahara watumishi 110 kupitia Mfuko wa Ruzuku,” alisema Dk. Fihavango.

Kwa uoande wake, mgeni rasmi ambaye alimwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika ibada hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika, alitoa pongezi kwa KKKT kwa kushirikiana na Serikali kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema Serikali inatambua mchango wa kanisa hilo katika kutoa huduma za kiroho, afya, elimu na uchumi bila kubagua wananchi kwa kigezo cha utofauti wa dini, hivyo limekuwa na mchango katika maendeleo ya taifa na kulitaka kuwahimiza waumini wake kutokwepa kulipa kodi ili Serikali ipate fedha za kuendesha shughuli za maendeleo.

“Katika kutoa huduma za afya, Serikali inaendelea kushirikiana na kanisa kutoa huduma hiyo kupitia Hospitali Teule ya Ilembula na Kituo cha Afya Kidugalo na zahanati nyinginezo ambazo ni mali ya KKKT Dayosisi ya Kusini,” alisema Mkuchika

Alisema Serikali inatoa vifaa tiba na mishahara kwa watumishi wa Hospitali Teule ya Ilembula ambao 110 ni wa kanisa na 37 wa Serikali ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za matibabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Shoo alimpongeza Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuwaletea Watanzania maendeleo katika sekta ya afya, elimu na nishati.

Alisema Rais Magufuli amerejesha nidhamu ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kwani nidhamu ya watumishi wa umma imekuwa ni chachu ya maendeleo katika taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here