AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM
WAKATI baadhi ya watu wakilalamikia huduma zinazotolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili –Mloganzia, Waziri wa Afya, Maendeleao ya Jamii, Jinsi,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema madai hospitali hiyo si ‘chinjachinja’ kama baadhi wanavyoiita.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati alipofanya ziara katika hospitali hiyo, Waziri Ummy aliwataka wananchi kuiamini hospitali hiyo kwani inatoa huduma bora kama zilivyo hospitali zingine.
“Nimefanya ziara ili kupata ukweli wa madai ya kwamba huduma zinazotolewa hapa ni mbovu, pia watu wameenda mbali na wengine kuanza kusema kuwa hiyo hospitali ni chinjachinja, mimi nataka kusema Mloganzila sio chinja chinja ni hospitali inayotoa huduma nzuri kama zilivyo hospitali zingine.
“Dhana iliyojengeka pale ni kwasababu ilivyoaanza ilianza kama hospitali ya kufundishia lakini na nyie mmeona Muhimbili, Bugando, KCMC kuna wanafunzi wanaojifunza, utaratibu wa wanafuzi kujifunza upo lakini utarataibu tuliokuta hapa ni kwamba daktari mwanafunzi anafanya kazi chini ya usimamizi wa daktari ambaye amesajiliwa na daktari bingwa.
“Kwahiyo mimi natoa rai kwa Watanzania tuwaamini madaktari wetu wanaofanya kazi katika hospitali ya Mloganzila, tuiamini hospitali ya Mloganzila inatoa huduma bora kama zilivyo hospitali kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,”alieleza Waziri Ummy.
Pia alisema licha ya mafanikio yaliyopo kwenye hospitali hiyo, kuna baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kutatuliwa.
“Changamoto kubwa nilioyoiona ni suala la usafiri lakini tunapongeza manispaa ya Ubungo kwa kujenga kituo cha mabasi usafiri utapatikana sasa, kunachanmoto ya mochwari hii ni kutokana na jinsi hospitali imejengwa ila nimeambiwa itaendelea kujengawa.
“Changamoto nyingine naomba hili wananchi walielewe hospitali imejengwa kama jengo la nchi zilizoendelea hivyo mgonjwa atakuja kuangaliwa na ndugu mmoja au wawili kwa siku ila katika utamaduni wetu wa kitanzani mgonjwa anakuja kuangaliwa na watu 10 hadi 20.
Kwa jinsi jengo lilivyo lazima tutumie lifti sasa lifti hiyo haiwezi kubeba watu wengi, hatuwaambii msiende kuangalia ndugu zenu, tutaangalia utaratibu wa kujenga sehemu ya kukaa ndugu wanaokuja kuangalia wagonjwa wao,”alibainisha .
Waziri Ummy alisema Serikali inaendelea kufanya mchakato wa matumizi ya lazima ya bima ya afya ili wananchi wote waweze kumudu gharama za matibabu.
“Na mimi natoa tena maelekezo kwa hospitali zote nchini ni marufuku mwananchi kukosa huduma kwasababu tu hana fedha za kutanguliza, nawapongeza Muhimbili kwa kuwa wanalizingatia na kutekeleza kwa asilimia 100.
“Ndio maana wakati mwingine kunatoka malalamiko ya kuzuia maiti lakini kwa hili tumeshatolea maelekezao watafute utaratibu mwingine wa kulipwa bila kuzuia maiti,”alieleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Profesa Lawrence Museru, ambaye pia ndiye msimamizi wa hospitali hiyo ya Mloganzila, alisema ututoaji wa mafunzo kwa watoa huduma za afya unafanyika hospitalini ili kuongeza ujuzi na ufanisi katika kazi .
“Kwahiyo Watanzania wakubali kuwa wapo wanaojifunza lakini anapojifunza hatumuachii maamuzi, atashirikiana na dakatari bingwa na ataona huyu anatakiwa kupata matibabu gani na anahali gani, tumekuja hapa kliniki tumekuta wataalamu wote hata wale wanafunzi hivyo ile dhana ya wagonjwa kutibiwa na madaktari wanaojifunza sio kweli,”alisema Prof Museru.