Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amemwagiza Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Abdallah Ikwasa, kumwondoa mara moja Meneja Uendeshaji wa Kituo cha Umeme Kidatu, Manfred Ndyalu kwa uzembe.
Mbali na hilo, pia amemtaka Mhandisi Ikwasa, Naibu Mkurugenzi Usafirishaji Umeme, Mhandisi Bishaija Kahitwa na Meneja Udhibiti Mitambo, Mhandisi Isihaka Mosha, kuachia nafasi zao endapo umeme hautarudi.
Dk. Kalemani alitoa maagizo hayo jana alipofanya ziara kwenye mitambo ya kuzalisha umeme Ubungo na Kinyerezi, Dar es Salaam baada ya kukosekana umeme nchi nzima, hasa kwa mikoa iliyoungwanishwa na gridi ya taifa.
“Nimetoka Dodoma leo (jana) kwa sababu haiwezekani umeme ukatike nchi nzima ndani ya saa 10 na bado hamjajua tatizo ni nini, wananchi wanatuma ujumbe mfupi kila kona wameunguliwa vitu vyao, wameunguliwa mashine zao, nani atalipa hizo gharama?
“Kutokana na vyanzo vya matatizo, tumechukua hatua kwamba Meneja Uendeshaji wa Kidatu hakutoa taarifa mapema ili kunusuru hali hii, huu ni uzembe, tumemwagiza mkuu wake amwondoe leo (jana) katika kituo hicho. Ili hali hiyo isijirudie tena, tuwe na wafanyakazi wachache wenye weledi,” alisema.
Awali akiwa katika kituo cha Kinyerezi I, baada ya kusikiliza maelezo kutoka kwa wataalamu, Dk. Kalemani alimtaka Mhandisi Ikwasa kuandika barua ya kujieleza ndani ya saa tatu, kwanini asiondolewe katika nafasi hiyo, huku akimpa siku tatu Mhandisi Mosha naye ajieleze.
“Siwaondoi, bali nataka umeme usiporudi muondoke wenyewe katika nafasi zenu, kwa sababu hii kazi itakuwa imewashinda.
“Hatuwezi kufanya kazi kwa mazoea, nataka kila mtu achape kazi kwa nafasi yake,” alisema.
Aliwahoji viongozi hao tatizo lilipo na wakamjibu kuwa kuna kifaa katika kituo hicho kimeyumba huku kwa upande wa Kidatu waya umeachia.
Kutokana na hilo, alieleza kushangazwa kwa kitendo cha spea za akiba za mitambo ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa umeme kutokuwapo.
Dk. Kalemani aliwahoji iwapo kulikuwa na hitilafu kwenye gridi ya taifa, ni kwanini mashine nyingine nazo zipoteze mwelekeo, huku kukiwa na kitengo cha mfumo wa uendeshaji.
“Hakuna haja ya kuwa na mfumo ambao hautoi taarifa mapema kama kuna tukio hatarishi linakuja, ninachotaka kusikia ni nini kifanyike ili tuwe na taarifa mapema.
“Kila mnaloulizwa hamjui, mnasubiri hadi mitambo iharibike ndipo mchukue hatua, nchi haiwezi kuendeshwa hivyo, kukosa umeme ndani ya saa 10 ni hatari kwa mali za raia, lakini kwa usalama pia.
“Sitaki kubishana, hilo ndilo neno ninalowaacha nalo leo, nataka umeme urudi nchi nzima, nina ‘detail’ za kutosha, hii haiwezekani,” alisema Dk. Kalemani.
Pia aliagiza mkandarasi anayeshughulikia mfumo wa utendaji wa umeme ambaye yupo nje ya nchi, kurudi nchini na hatarudi Dodoma hadi ajue hatima yake.
Baada ya ziara hiyo, Dk. Kalemani alikutana na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa baada ya kufuatilia, wamegundua kuwa tatizo la kukatika kwa umeme limesababishwa na kukatika kwa waya wa kupelekea umeme kwenye geti la kufungulia maji katika bwawa la Kidatu.
“Hitilafu hiyo ilisababisha mtambo wa Kidatu pamoja na mitambo mingine ya kuzalisha umeme katika sehemu mbalimbali nchini kutoka kwenye Gridi ya Taifa kuharibika na hivyo kusababisha mikoa yote iliyounganishwa kwenye mfumo wa gridi hiyo kukosa umeme.
“Mtambo wa Ubungo II wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 129, utaanza kuzalisha umeme ifikapo kesho (leo) asubuhi,” alisema.
Alisema wanaendelea kuchukua hatua za dharura ikiwapo kukarabatiwa kwa mitambo yote ya kuzalisha umeme iliyoharibika ndani ya kipindi cha wiki mbili.