26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MVUA YA KISHINDO

Waandishi wetu

MVUA zilizonyesha kwa kishindo ndani ya siku mbili, zimeleta balaa Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo vya watu wawili.

Pia mvua hizo zimesababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara, nyumba kubomoka na hali ya usafiri kuwa ngumu kwa jana.

Hata hivyo, katika maeneo ya baadhi ya mikoa ya Pwani, mvua hizo zimekuwa neema kwa wakulima na wafugaji ambao mifugo yao ilianza kudhofika kutokana na ukame.

Baadhi ya wafugaji hao wamesema katika maeneo ya Vigwaza na Chalinze, mifugo ilikuwa imeanza kudhoofika na kuwa na wasisi wa kupoteza mifugo mingi kama ilivyokuwa wakati wa ukame wa mwaka jana hadi Februari mwaka huu.

“Sasa hivi maji tayari yamejaa kwenye malambo, tunaimani ndani ya juma moja nyasi zitakuwa zimeanza kustawi kwa hiyo wasiwasi wa mifugo yangu kufa imeisha kabisa,” alisema mfugaji mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Kauli ya TMA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Uendeshaji Vituo vya Hali ya Hewa Tanzania, Hellen Msemo, alisema mvua zinazoendelea kunyesha zitanyesha kwenye mikoa yenye misimu miwili ya mvua.

“Mvua zinazoendelea kunyesha ni za vuli ambayo ni mahsusi kwa mikoa ambayo inapata misimu miwili ya mvua kama vile Dar es Salaam, Tanga, Pemba na Unguja, Morogoro, Kilimanjaro, Kagera na mingine.

“Jumanne TMA alitoa utabiri wake kwamba kutakuwa na mvua kubwa siku ya Jumatano na Alhamisi hivyo watu wachukue tahadhari. Tunatarajia kesho (leo) hakutakuwa na mvua kubwa hivyo itanyesha ya kawaida tu,” alisema Hellen.

Aidha aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA kuhusu utabiri wa hali ya hewa na kuchukuwa tahadhari pindi wanapohitajika kufanya hivyo.

Polisi

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliliambia gazeti hili kuwa mvua hiyo imesababisha vifo vya watu wawili kwenye maeneo ya Tabata na Mbezi Luis.

“Bado tupo eneo la Jangwana tunaendelea kuokoa watu waliozungukwa na maji, tathimini nyingine tutatoa baadaye” alisema Mambosasa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema, aliwataka wananchi wa eneo la jangwani kuodoka eneo hilo na kwenda kutafuta hifadhi katika maeneo salama hadi hapo hali itakaporejea vizuri.

Aliwataka kuhakikisha wanachukua hadhari kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuwazuia watoto kwenda shule kama njia wanazotumia zitakumbwa na mafuriko.

“Ukiangalia karibu na klabu ya Yanga asilimia 80 au 90 ya nyumba zote zimezingirwa na maji na yamejaa hadi ndani, kwa hiyo ni vema hata wasilale hapa” alisema DC Mjema.

Naye Mbunge wa Ilala, Musa Azzan Zungu, alisema kinachoendelea kwa sasa ni kuhakikisha wananusuru maisha ya wananchi wa maeneo hayo kwa kupata namna ambayo wanaweza kuitumia kufungua njia za maji ili yapungue katika eneo la Jangwani ili kuwezesha magari kupita.

“Mvua hii ni kubwa mno kwa siku za karibuni hali iliyosababisha madaraja kujaa mchanga na takataka na kuziba hivyo kushindwa kupitisha maji” alisema Zungu.

Alisema wanaendelea kutafuta mtambo wenye uwezo wa kungia majini ili kuzibua daraja hilo ili kurejesha barabara katika hali yake ya kawaida.

Mbezi

MTANZANIA lilifika maeneo ya Mbezi Kibanda cha Mkaa majira ya saa tano na kukuta maji yakiwa yanapita juu ya daraja na hivyo wasafiri waliokuwa wakitoka maeneo ya Kibamba, Mbezi kuelekea Ubungo na kati kati ya mji kukatisha safari.

Inocent Marko, aliyekuwa eneo hilo alisema. “Maji yalianza kupita hapa kwenye saa nne, kuvuka hapa sasa hivi haiwezekani kama unavyoona, kuna gari aina ya Hiace limesombwa na maji wakati linapita ingawa watu waliokuwamo wameokolewa,” alisema.

Pia katika eneo la Mbezi Luis, daladala jingine lilisombwa na maji ingawa waliokuwa katika eneo hilo waliokolewa.

Daraja linalounganisha Mtaa wa Mazulu Msikitini na Mtaa wa Kilima Hewa Kata ya Mbezi Mwisho lilisombwa na maji, hivyo kusababisha mawasiliano ya wakazi wa pande hizo mbili kukatika.

Mtanzania lilizungumza na Mkazi wa Mtaa wa Mazulu Msikitini, Asha Bamali alisema. “Hali ndiyo kama inavyoonekana kwani kwa kadiri mvua inavyoongezeka hali inazidi kuwa mbaya na si kusema eti sisi tumefuata mkondo wa maji lakini maji yametufuata.

“Daraja hili linaunganisha mtaa huu na Kilima Hewa hivyo kutokana na hali ya kusombwa na maji hakuna mawasiliano tena. Na ninavyozungumza watoto wetu wapo shuleni na hii ndio njia yao hatujua tutafanya nini hivyo tunaiomba Serikali ifanye jitihada za mapema sana kuangalia namna ya kutatua changamoto hii,” alisema Asha.

Jangwani

Katika eneo la Jangwani, maji yalionekana kufurika kiasi cha kufunga barabara ya Morogoro na kufanya eneo hilo lisipitike.

UDART yasitisha huduma

Kutokana na hali hiyo, Kampuni ya inayotoa huduma kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha kampuni hiyo, Deus Bugaywa ilitangaza kusitisha huduma zake kutokana na kufungwa kwa barabara ya Morogoro kutokana na mafuriko.

“Kutokana na kufungwa kwa Barabara ya Morogoro kwa sababu ya Daraja la Mto Msimbazi kujaa maji hivyo huduma itarejea mara baada ya hali kutengemaa. Tunawaomba radhi abiria wetu kwa usumbufu uliojitokeza,” alisema  Bugaywa.

Abiria Dar – mikoani wakwama

Katika hatua nyingine, abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea Dar es Salaam kutoka mikoa mbalimbali na wale waliotoka Dar es Salaam kwenda mikoani, kutumia barabara ya Morogoro walijikuta wakikwama kwa takribani saa 12 kutokana na daraja  linalotenganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kujaa maji.

Kufuatia hali hiyo watu watano waliokuwa wakijaribu kuvuka katika daraja hilo wakati maji hayo yakiwa yamejaa, walisombwa na maji na kuokolewa.

Uokoaji wa watu hao ulifanyika kwa ushirikiano wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Pwani, Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani, askari Magereza na wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Mpaka saa 11 jioni jana, kulikuwa hakuna gari lolote lililoruhusiwa kuvuka katika daraja hilo ambapo maji yalikuwa yanasubiriwa kupungua kwenye daraja hilo ili likaguliwe kama limeathiriwa kiasi gani na mvua hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles