|Bakari Kimwanga, Morogoro
Mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge, unatarajiwa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 ambazo zinatarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Meneja mkuu wa Kampuni Tanzu ya Tanesco- ETDCO, Mhandisi Elangwa Mgheni Abubakar, amesema kwa sasa kazi ya ujenzi inayoendelea ni usimikaji waya maalumu zenye madini ya kopa kutoka katika kituo cha Matambwe hadi kwenye eneo la mradi.
Pamoja na hali hiyo alisema kutokana na ukubwa wa mradi huo wa kihistoria nguzo zitakazotumika kwa mara ya kwanza ni za zege zaidi ya 700.
“Mradi mzima utakuwa na nguzo za zege 700 zenye urefu wa milimita 17. Na huu ni mradi wa kwanza kutumia nguzo za aina hii.
“Tunaendelea na ujenzi huu huku tukiwa tumezingatia masharti ya kitaalamu ikiwamo kukata miti bila kuathiri mazingira kutoka usawa wa ndege.
“Kwa sasa kazi inayoendelea mafundi wanalaza kebo ambayo itazunguka na kupita chini ya reli na daraja, awamu ya pili itakuwa kama ya ujenzi pia tutaweka kebo.
“Hii line itabeba 33 KV na ya pili nayo itakuwa na ukubwa kama huo ambayo ndani yake kuna waya wa kopa pamoja na nyaya zake ambazo ni nzito,” amesema Mhandisi Elangwa.