24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Umeme jua unavyotumika kumwagilia mbogamboga

pichaNA ELIYA MBONEA, ARUSHA

KIWANGO cha uzalishaji wa mbogamboga na matunda nchini kinatarajia kuongezeka zaidi baada ya wakulima wa bustani kuanza kutumia Teknolojia ya Umeme wa Jua kumwagilia mazao yao.

Teknolojia hiyo imekuwapo nchini kwa miaka mingi sasa, japo ilijielekeza kujibu changamoto za ukosefu wa mwanga kwenye makazi ya watu wasiounganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.

Kutumika kwa umme huo, hakukuwa kwa waliopo vijijini tu, bali umeme huo umeendelea kutumika maeneo ya mijini kama kinga ya kukatika kwa umeme lakini pia gharama zake zikitajwa kuwa ni nafuu.

Mbali na matumizi na unafuu wake, teknolojia hiyo imeendelea kuimarika kwa kuibuka kampuni mbalimbali zinazotengeneza bidhaa zitumiazo umeme wa jua kama ambavyo zingeweza kutumia umeme unaotengenezwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Katika mabadiliko hayo, leo tunashuhudia au kununua bidhaa zinazotumia umeme wa jua kama redio, luninga, jokofu yakiwapo pia matumizi ya kuchemshia maji, kuchaji simu na mambo mengine mengi.

Kujibiwa kwa mahitaji ya mwanga na bidhaa zinazotumia umeme wa jua, sasa kupitia teknolojia hiyo kumeanza kujibu changamoto zinazowakabili wakulima wa bustani.

Kama ilivyo kwa watu waliohitaji mwanga usiku, ndivyo ilivyo kwa wakulima wengi wanaoendelea kutumia muda, fedha na nguvu nyingi kuhamisha maji eneo moja hadi ulipo mmea kwa ajili ya kuumwagilia.

Changamoto hii si tu imewagharimu wakulima huko vijijini, bali pia imewalazimisha kulima maeneo wanayoweza kuyahudumia hasa kwenye umwagiliaji na mambo mengine ya shambani.

Kwa mfano, wakulima wa mazao ya bustani Kijijini Mtule, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja wao wamechimba visima na hupandisha maji kwenye tenki kwa kutumia jenerata ili baadaye yaelekezwe ulipo mmea kupitia mirija yenye matundu (Drip Irrigation).

Mkulima wa nyanya kijijini hapo, Issa Kamata, anasema kupandisha maji kwenye tanki kwa kutumia jenereta kunatumia gharama kubwa kiasi cha kuwafanya washindwe kufikia malengo waliyojiwekea.

“Tunaiomba Serikali na wadau wengine watufungie umeme ili tuutumie pia kumwagilia mazao yetu, kwa sasa tunatumia gharama kubwa kununua mafuta ya petroli,” anasema Kamata.

Iddi Hassan mkulima wa tikiti maji eneo la Kiembeni Kitongani, yeye anasema huvuta maji kwa mpira kutoka kisimani kisha kuyahifadhi kwenye tanki mbadala alilotengeneza kwa miti na mifuko ya plastiki.

Changamoto haiishi kuhifadhi maji bali anasema huendelea kutumia muda mwingi na nguvu za kuchota maji kwenye tanki na kuyapeleka ulipo mimea.

“Natumia nguvu na muda mwingi ndiyo maana nimelima eneo ambalo halitanizidi nguvu kwenye umwagiliaji. Kama ningepata msaada wa kujengewa tanki la juu naamini lingenisaidia zaidi,” anasema Hassan.

Wakati wakulima hao wakionyesha kiu ya kupata nishati itakayosaidia kusukuma maji shambani, hali hiyo ni tofauti na mkulima aliyepo katika Kijiji cha Umbuji, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini, Visiwani Zanzibar.

Mkulima Fakh Hanaf anayelima pilipili hoho, tikiti maji, matango na bamia, anasema Asasi Kilele ya Kilimo cha Bustani nchini (TAHA) imemwezesha kupiga hatua zaidi.

Anasema kitendo cha kufungiwa umeme Jua ‘Solar Panel’ na pampu ya kupandisha maji kwenye tanki kisha kuyashusha shambani kupitia mirija kumeongeza kasi ya uzalishaji na kumpunguzia gharama alizozitumia awali.

Hanaf anasema pampu huvuta maji kutoka kisimani kwa saa 1 hadi 2 ambapo tanki huwa limejaa.

“Tanki likishajaa ninazima upande wa kisima na kuiacha wazi sehemu ya tanki ambako maji husukumwa na pampu hiyo kuelekea shambani kwa siku nzima.

“Nawashukuru sana TAHA bila wao ningeendelea kutumia majenereta na mipira minene ya kumwagilia ambayo ni gharama kwetu wakulima wadogo,” anasema Hanaf.

Kabla hajaanza kutumia umeme wa jua Hanaf anasema, alikuwa akimwagilia mazao yake kwa kutumia Cane kwenye eneo la hekari moja ambapo alitumia saa 6 kwa vibarua watatu.

“Vibarua niliwalipa Sh 100,000 kwa mtu mmoja kwa mwezi, lakini tangu TAHA wamenifungia teknolojia hii nimepunguza gharama na mahitaji mengine.

“Sihitaji mipira mikubwa, jenereta au kutumia cane, nimefunga mipira myembamba inamwagilia siku nzima kwa kutumia umeme wa jua. Kilichopo hapa ni kuwasha tu shughuli inaendelea,” anasema.

Anasema katika eneo la nusu hekari kwa msimu mmoja huvuna pilipili hoho polo 144 (Polo ni mfuko wa Kilogram 45). Mfuko mmoja huuzwa kati ya Sh 60,000 hadi 70,000.

Hanaf anasema polo moja ina uzito wa kuanzia kilogram 27 na huuzwa kati ya Sh 2,500 hadi Sh 3,000 kwa kilogramu moja.

Kuhusu gharama anazotumia kuotesha zao hilo, anasema hununua mbegu mifuko 10 kwa Sh 300,000, mbolea ya kuku mifuko 30, ambapo mfuko  mmoja huuzwa Sh 2,500, mifuko 30 ya mbolea popo kwa Sh 1,000 kwa mfuko.

Anasema mbali na gharama hizo pia hulazimika kulipia vibarua Sh 120,000 kwa ajili ya kumtengenezea matuta na baada ya hapo hulipia tena Sh 60,000 ya vibarua wa kufukua mashimo.

“Mbolea ya kupandia huwa naichanganya kwenye maji na kuikweka kwenye tanki. Lakini mbolea ya kuku na popo hii naweza kuendelea kuiweka hata mara tatu mpaka nitakapokuwa navuna,” anasema Hanaf.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, anayeshughulikia kilimo, Juma Ali Juma, anasema wameanza kutumia nishati mbadala ya umeme wa jua ili kusaidia wakulima.

“Teknolojia hii tunaendelea kuichangamkia ili ipunguze gharama na kuongeza tija na kipato kwa wakulima wa mbogamboga na matunda,” anasema Juma ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya TAHA.

Anasema kwa miaka mingi wakulima wameendelea kuzalisha mbogamboga na matunda kwa kutumia injini za mafuta na kwa msimu mmoja hutumia wastani wa Sh 900,000 kuvuta maji na kumwagilia shambani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles