Na GAMALIEL LAITON,
KABLA ya kufanyika Mkutano wa Berlin mwaka 1884 hadi 1885, Somalia ilikuwa ni himaya thabiti iliyoungana na yenye nguvu, chini ya miunganiko ya koo mbalimbali zilizokuwa zimeunganishwa na lugha moja na imani moja ya Kiislamu (imani ya Kisuni).
Mkutano huo wa Berlin uliigawa Somalia vipande vipande, Kusini, Kaskazini, Magharibi na Mashariki, mithili ya tsunami ivurugavyo mambo.
Mpakani mwa Ethiopia eneo kubwa la Ogaden na Haud lilitwaliwa, Djibouti likatwaliwa na Ufaransa na upande wa mpakani mwa Kenya Somalia ikamegwa na kuundwa kwa kile kilichoitwa Somalia ya Kusini.
Nia ya kuiunganisha Somalia tena ilikuja kufufuliwa na Jemedari Mohamed Siad Barre, aliyeingia madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwaka 1969.
Siad Barre alikuwa muumini wa ujamaa, utawala wake uligubikwa na udikteta na mkono wa chuma, aliojitahidi kuutumia kuirudisha Somalia iliyokuwa imepotezwa na mataifa ya Magharibi karne ya 19, akijua kuwa mbegu ya mtengano na kuchafuka kwa Somalia ni mgawanyiko ndani ya roho za Wasomali wenyewe, chanzo kikiwa ni farakano lililosababishwa na ubaguzi wa koo na koo.
Siad alichukua hatua mbalimbali dhidi ya ubaguzi huo, kwa mfano alipiga marufuku Salamu za kikabila/kikoo zilizokuwa zimeshamiri (koo na koo zilikuwa na salamu zake pekee zikitaja maneno, hususan kutambulisha koo fulani dhidi ya koo nyingine).
Alichukua hatua nyingine madhubuti ya kuhakikisha jeshi linaundwa kwa usawa baina ya koo zote, bila kupendelea vyeo kwa koo fulani.
Wakati Siad Barre akipambana na ubaguzi ndani ya Somalia, kuna kansa nyingine iliyokuwa ikiinyemelea Somali, ‘Nafasi ya Somalia kati ya mataifa mawili makubwa’ katika vita baridi iliyokuwa ikipiganwa baina ya Muungano wa Sovieti na taifa hasimu Marekani.
Mwaka 1974 Somalia ilikuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kusaini mkataba wa kijeshi na Muungano wa Sovieti, mkataba uliohusisha ushirikiano wa kijeshi baina ya Somalia na muungano wa Sovieti.
Muda mfupi baada ya mkataba huo, kundi la wanajeshi zaidi ya 6,000 kutoka Muungano wa Kisoviet walikuwa tayari wako katika ardhi ya Somalia.
Inasemekana Somalia iligeuka kama Kremelin (Ikulu ya Muungano wa Sovieti) ndogo, kwa muda mfupi jeshi hilo dogo lilichukua hatamu katika wizara nyeti kama vile wizara ya ulinzi, habari na mambo ya ndani, kwa muda mfupi Jeshi la Somalia likageuka kutoka jeshi dhaifu hadi jeshi la wanajeshi zaidi ya 27,000 wenye uwezo wa kutumia silaha kali za kivita na uwezo wa kutumia bunduki kama AK47.
Shule na madrasa zikageuzwa kuwa vituo vya kufundisha sayansi ya siasa badala ya hesabu na kujua kusoma.
Hali ya uwepo wa majeshi ya muungano wa Kisovieti katika ardhi ya Somalia ilikuwa ni habari mbaya kwa taifa la Marekani, likitambua hatari ya kupanuka kwa Muungano wa Sovieti, Marekani ikafanya kila linalowezekana kuwa na kambi ya kijeshi katika nchi jirani ya Ethiopia.
Kumbuka katika mkutano wa Berlin eneo la Haud na Ogaden, eneo lililokuwa la Somalia lilimegwa kutoka Somalia na kuwekwa chini ya Ethiopia.
Mwaka 1977 Somalia chini ya Siad Barre na msaada wa majeshi ya muungano wa Sovieti, ikavamia Ethiopia, lengo likiwa kukomboa eneo la Ogaden na Haud, vita iliyoiachia ushindi Somalia kwa kufanikiwa kukomboa asilima 99 ya eneo la Ogaden na Haud, Ethiopia na mshirika wake Marekani wakashindwa.
Wakati huo Muungano wa Sovieti ulikuwa na malengo ya mengine zaidi, ikaanza kufadhili vijana nchini Ethiopia, waliompindua mtawala Haile Selasie.
Baada ya mapinduzi, Sovieti ikaanza kumlazimisha Siad Barre aunde serikali ya muungano ya kijamaa na Ethiopia, jambo ambalo halikumuingia Siad Barre kichwani kwake.
Kutoelewana baina ya Sovieti na Somalia kukaanzia hapa, kwa muda mfupi uhusiano baina ya Siad na Serikali ya Kremlin ukadhoofu, hatimaye kufa.
Sovieti ikahamisha nguvu zake nchini Ethiopia, kama vile wachezaji wa mpira wa miguu wabadilishanavyo magoli wakati wa mapumziko. Marekani ikahama uwanja toka Ethiopia na kuhamia Somalia, huku Muungano wa Sovieti nao ukihama kutoka Ethiopia na kuhamia Somalia.
Siad Barre alikuwa akitoka ukoo mkubwa wa Marehani, kadiri muda ulivyokuwa ukipita, akaanza kuwapendelea watu wa ukoo wake katika vyeo vya kijeshi, hali iliyozua manung’uniko kutoka koo nyingine kama za Habr, Gedir na Abgar.
Mwaka 1990 muunganiko wa hayo makabila matatu chini ya Jenerali Mohamed Farah Aidid (kutoka muungano wa koo za Habr na Gedir) na Ali Mahdi kutoka koo ya Abgar ukaungana kumpindua Siad Barre.
Januari 1991 Siad Barre akatorokea nchini Kenya, muda mfupi tu baada ya Barre kukimbia, Ali Mahdi akajitangaza kuwa rais kinyume na makubaliano yaliyokuwapo baina yake na Jenerali Aidid.
Ali Mahdi alikuwa ana mtaji wa watu kutokana na ukubwa wa koo yake, Jenerali Aidid alikuwa na mtaji wa silaha za kivita, kutokana na mfarakano baina ya Aidid na Ali Mahdi kukazua vita baina ya koo hizo mbili na kuigawa Somalia vipande viwili Somalia ya Kusini na Kaskazini. Kipindi hicho Somalia ikakumbwa na njaa kali iliyotangazwa duniani kote, picha za televisheni zikipambwa na Wasomali waliokonda na kubaki mifupa mitupu, ni wakati huo Umoja wa Mataifa ulipoingia Somalia na ile Operesheni iliyoitwa ‘Rudisha Tumaini’.
Operesheni hiyo ilipokelewa kwa mitutu na ukinzani kutoka kwa mabwana wa vita Aidid na wenzake, ni wakati huo ile helikopta ya Marekani iliyoitwa ‘Black Hawk’ ilipodondoshwa na rubani wake kutekwa na kuuawa, ni wakati huo picha za televisheni zilisambazwa duniani, ikiwamo ile video ya maiti za wanajeshi wa Marekani wakiburuzwa katika barabara za Mogadishu.
Mgawanyiko wa koo, kugawanywa vipande vipande na mataifa ya nje, kuathirika kisaikolojia kutokana na vita, mazingira magumu ya jangwa na ukame, visasi baina ya koo, kiu ya madaraka, usaliti, unafiki wa Umoja wa Taifa, kutoaminiana baina ya Wasomali wenyewe.
Haya yote ndiyo yanayosababisha Somalia kuwa kama ilivyo leo. Hii ndiyo Somalia anayorithi Mohamed Abdullahi Farmajo, Rais mpya wa Somalia.
Farmajo alizaliwa Mei 5, 1962 mjini Mogadishu, Somalia (anatoka kabila la Merehani, kabila moja na Siad Barre), ni mwanadiplomasia na Profesa na Rais wa Tisa wa Somalia.
Farmajo alipata kuwa Waziri Mkuu wa Somalia mwaka 2010 hadi 2011, mwaka huu Farmajo alichaguliwa kuwa rais wa Somalia baada ya kupata kura 184 dhidi ya kura 328 za wawakilishi.
Farmajo ana uraia wa nchi mbili, Marekani na Somalia, alishawahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, kuanzia mwaka 1994 hadi 2009. Kabla hajachaguliwa kuwa waziri mkuu nchini Somalia (mwaka 2010), Farmajo alifanya kazi mbalimbali nchini Marekani katika sekta ya usafiri.
Juni 19, 2011, Farmajo alijiuzulu uwaziri mkuu baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na Bunge la Somalia, baada tu ya kujiuzulu alirudi nchini Marekani na kuendelea na maisha yake kama raia wa nchi hiyo.
Shaka yangu kama Farmajo ataweza kuleta mabadiliko ndani ya Somalia wakati kukiwa na mpasuko, je; ataiweza Somalia? Kama tulivyoona hapo juu wasifu wa Farmajo mwenyewe, ametumia zaidi ya nusu ya maisha yake nchini Marekani, pia ana uraia wa Marekani, hana la kupoteza iwapo Somalia itaendelea kuyumba ama kuimarika.
Rais huyo ana uhakika wa kurudi nchini Marekani kama alivyofanya baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu. Kama tulivyoona pia historia fupi ya Somalia ilivyopitia katika mgawanyo na kutoaminiana wenyewe kwa wenyewe, je, Farmajo ataweza kweli kuiunganisha tena Somalia? Farmajo anatoka kabila moja na Siad Barre, aliyeshindwa kuiunganisha Somalia kwa mkono wa udikteta na ujamaa wa kisovieti, kabla Somalia haijagawanyika tena vipande viwili.
Shaka nyingine ni kutokana na Farmajo kuwa pandikizi au amali (asset) ya Marekani.
Shaka hii kwanza inatiwa nguvu na uraia wa Farmajo mwenyewe, ni raia wa Marekani. Pili, yeye mwenyewe ni muhimu kwa Somalia yenyewe.
Katika enzi hizi na katika historia bahari imekuwa ni alama muhimu ya utawala wa soko na siasa za dunia, taifa linalomiliki bahari ndilo linalomiliki misafara ya biashara na shughuli zote zinazofanyika juu na ndani ya bahari, miaka ya nyuma taifa lenye kumiliki bahari ya Atlantiki ya Kaskazini ndilo lilikuwa likitawala dunia. Mataifa mengi ya Ulaya yamepigana vita kubwa na kuingia katika mizozano mikubwa juu ya umiliki wa njia za Bahari ya Atlantiki ya Kaskazini, kwa kuwa karne kadhaa zilizopita misafara ya biashara zote ilikuwa inapita katika bahari hii.
kuanzia miaka ya 1980 kwa mara ya kwanza biashara zikaanza kufanyika kupitia Bahari ya Pasifiki na umuhimu wa Bahari ya Atlantiki ya Kaskazini ukapungua. Ili nchi kama Japan na China zipate mafuta ya petroli kwa ajili ya magari na viwanda vyake, ni lazima meli kubwa za mafuta zipite katika ghuba ya Adeni na Pwani ya Somalia yenye kina zaidi ya maili 920 na upana wa zaidi ya maili 320, ikiambaa kutoka Yemeni hadi katika pembe ya Afrika (Somalia).
Asilimia 10 ya mafuta duniani yanapita katika ghuba na pwani, bidhaa zenye thamani za trilioni zinapita katika pwani ya ghuba hiyo kila mwaka.
Taifa lolote lenye hatimiliki katika ghuba na pwani hiyo litajihakikishia faida na nguvu ya kuweza kufanya biashara, nafasi ya kurandaranda kwa manowari na shughuli za kivita na usalama wa bidhaa zinazoweza kupita katika ghuba na pwani hiyo.
Taifa lolote kubwa na lenye mrengo wa kibepari kama Marekani haliwezi kuiacha Somalia iangukie kwa taifa kinzani, na hivyo ni lazima lifanye kila namna kuhakikisha linakuwa na mkono juu yake, na ninadhani kete waliyoitumia ni kuhakikisha wanatengeneza mazingira Farmajo ashinde urais nchini Somalia. Kama ni kweli Farmajo ni amali (asset) ya Mmarekani, kuna nafasi ndogo ya Somalia kusimama kwa miguu yake yenyewe na hivyo kumaliza matatizo yake yenyewe.
Sina hakika kama Marekani ina uchungu na Wasomali zaidi ya kuona masilahi ya pwani wa Somalia, nadhani amani na Somalia ya kweli itatoka ndani ya Wasomali wenyewe kuliko kusubiri taifa kama Marekani lipandikize rais wake na ndipo Somalia isimame.
Kipindi cha nyuma Siad Barre alijikuta hajui afanye nini baada ya kuachwa na Muungano wa Sovieti, baada ya kutokukubali kuwa mtumwa wa kufuata kila neno kutoka kwa Wasovieti, je, kama kweli Marekani iko nyuma ya Farmajo, atavumilia kuitikia ndiyo kwa kila neno kama punda wa dobi? Je, itakuwaje siku atakapochoshwa? Muda ni mwalimu mzuri, utahukumu.