26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ulinzi wa Mbowe mahakamaniwaitisha Chadema

Na GRACE SHITUNDU- DAR ES SALAAM

BARAZA Kuu la Vijana Chadema (Bavicha), limelinyooshea kidole Jeshi la Polisi kwa kutumia nguvu kubwa mahakamani wakati kesi za viongozi wakuu wa chama hicho zinaposikilizwa.

Kutokana na hilo, Bavicha imelitaka Jeshi la Polisi kutoa tamko endapo kwenda kusikiliza kesi ya viongozi wa Chadema ni haramu.

Aidha, wameutaka uongozi wa mahakama kueleza iwapo mahakama hiyo imekuwa ya kijeshi kutokana na kuwa na ulinzi mkali wakati wa kesi hiyo.

Viongozi wanane wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

Mbowe pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, wako rumande baada ya kufutiwa dhamana.

Viongozi wengine wanaotuhumiwa katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Kauli ya kulituhumu Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi, ikiwa ni siku moja baada ya kesi ya viongozi hao namba 112/2018 kuahirishwa hadi Desemba 21, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.

Akizungumza na vyombo vya habari, Sosopi, alisema wamefuatilia tangu kuanza kwa kesi hiyo Machi mwaka huu kwamba kuna desturi mpya ambayo jeshi hilo limeanzisha ya kutumia nguvu nyingi wakati kesi inayowakabili viongozi wao wakuu inapotajwa katika mahakama ya Kisutu.

“Mahakama ni ‘public office’ (ofisi ya umma) ni ofisi za kiserikali zinazohudumia wananchi, lakini Jeshi la Polisi linatumia nguvu kubwa kila wakati kesi ya viongozi wetu inapotajwa mahakamani.

“Kuzuia watu kwenda kusikiliza mashauri yanayoendelea katika mahakama na ni haki ya msingi, lakini nguvu kubwa inayotumika na Jeshi la Polisi na mazingira ya mahakama yanayokuwa wakati kesi hizo zinapokuwa zikiendelea zinakuwa kama mahakama za kijeshi,” alisema Sosopi.

Alisema hali hiyo inawazuia hata wananchi wengine ambao wanahitaji huduma ya kuwawekea dhamana baadhi ya watuhumiwa.

“Lakini pia kutoa ushahidi na hata kusikiliza kesi za ndugu zao, kwa kuwa kuna kesi ya kina Mbowe basi wanazuiwa,” alisema.

Alisema kama haitoshi juzi waliwakamata vijana wa Chadema zaidi ya 10 katika eneo la Mahakama.

Kwa mujibu wa Sosopi, vijana hao walikwenda kusikiliza kesi inayowakabili viongozi hao wakuu wa Chadema.

Wakati huo huo Baraza hilo limewaomba wananchi kwenda magerezani kuwatembelea wafungwa ikiwa ni maadhimisho ya kusherehekea siku ya Uhuru.

WASIKITIKA SHEREHE ZA UHURU KUFUTWA

Aidha, Baraza hilo limesema limesikitishwa na hatua ya agizo la kuondolewa sherehe za uhuru zilizokuwa zifanyike Dodoma kwa mwaka huu lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli, kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Sosopi alisema kwa kuziondoa sherehe hizo kutawafanya wananchi hasa vijana wanaokuwa kutokuona umuhimu wa sherehe hizo.

“Sherehe za uhuru ni muhimu kuliko sherehe za kukimbiza mwenge ambazo humaliza fedha nyingi kila mwaka,” alisema Sosopi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles