Maeneo ya Ulaya yameanza mchakato mrefu wa kufungua upya nchi zao baada ya kufungwa kutokana na virusi vya corona jana, lakini maambukizi mapya katika muda wa wiki kadhaa nchini China yanatoa ishara ya wasi wasi juu ya hatari ya wimbi la pili la kesi za maambukizi.
Hali hiyo inaonesha jinsi Serikali zinavyokabiliwa na hali ya hatari duniani wakati zikijaribu kufungua uchumi wao wakati huo huo zikijaribu kudhibiti janga hilo ambalo sasa limekwisha wauwa zaidi ya watu 280,000 duniani kote.
Wakati Uingereza ikipanga njia kuelekea hali ya kawaida na Ufaransa na Uhispania zikiingia katika hali ya kulegeza vikwazo, mji wa China ambako janga hilo lilianzia uliripoti siku ya pili ya maambukizi mapya baada ya mwezi mmoja bila ishara za virusi hivyo.
Karibu wiki saba baada ya amri ya kubakia majumbani kuwekwa zaidi ya watu 31,800 wamefariki nchini Uingereza, idadi ambayo ni ya pili tu baada ya Marekani.
Idadi ya kesi za maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani iliongezeka kwa watu 357 hadi watu 169,575, data kutoka katika taasisi ya Robert Koch zimeonesha.