28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

UKITAKA KUBADILI MAISHA YAKO, ANZA KUBADILIKA WEWE KWANZA

happy-lady

Na ATHUMANI MOHAMED

WATU wengi ni mabingwa wa kulalamika maisha magumu. Wapo watu ni mabingwa kwelikweli wa kulia kila siku hawana pesa, madeni yanawaandama nk.

Wapo wengine wamekuwa wakilalama kwamba, maisha yao ni magumu kwa sababu hawajasoma. Utakuta mtu anasema: Ooooh! Mimi sina maisha mazuri kwa sababu sina kazi ya maana.

Ndugu yangu, katika maisha haya hakuna anayeridhika. Kuna watu wanafanya kazi nzuri, mishahara yao ni milioni sita mpaka saba, lakini wanalalamika maisha magumu.

Pia usisahau kuwa kuna wengine wanalipwa hadi milioni 12 kwa mwezi, lakini ukimwuliza kuhusu mshahara wake, atakuambia analipwa kidogo na anataka kampuni anayofanya kazi ifikirie kumuongezea.

Ndivyo ilivyo. Muhimu katika maisha ni kujikubali katika hali uliyonayo kisha uanzie hapo. Kamwe huwezi kurudi tena tumboni mwa mama yako ukazaliwa upya ili ukutane na mzazi mwenye fedha za kukukosomesha, uwe na kazi nzuri.

Hata kama wazazi wako wameshafariki dunia na pengine unawaza kwamba wangekuwepo wangekusaidia, kamwe hawawezi kufufuka leo hii wakusaidie. Inawezekana wazazi wako hawakukusomesha, kwa sababu maisha yalikuwa magumu na wakakosa fedha za kukulipia ada.

Ni sawa… sasa utalazimisha? Kama walikosa kweli? Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba hawakukudhuru. Walikulea kwa tabu hadi sasa ni mtu mzima mwenye utashi wako. Hilo kwanza unapaswa kumshukuru sana Mungu.

Mabadiliko ya maisha yako ni lazima. Unachopaswa kufanya ni kuanza kufikiria kisasa. Achana na tabia za kufikiria kizamani. Fikiria kisasa kwa kuacha yaliyopita yabaki nyuma yako, huku wewe ukisonga mbele.

ACHA KULAUMU

Huna sababu ya kulia kuhusu wazazi wako waliofariki, lakini pia hakuna haja ya kulalamika kuwa hujasoma. Kama wewe ni mtu mzima na bahati mbaya kwa sababu za kifamilia hukusoma, bado una nafasi.

Je, ndoto zako za mafanikio zinahusisha elimu? Kama ndivyo, fahamu kuwa elimu haina mwisho. Kwa ngazi yoyote uliyopo unaweza kujiendeleza. Mfano umeishia kidato cha nne, angalia fani unayotamani kusomea, nenda chuo – omba kuingia masomo ya jioni.

Timiza ndoto zako. Huna haja ya kulaumu wazazi wako. Wao walijitahidi kutimiza majukumu yao kwa uwezo wao na kwa namna walivyoweza. Walipofikia ndiyo uwezo wao, usilazimishe kurudisha wakati nyuma.

JICHUNGUZE UNAVYOISHI

Angalia kwa makini sana namna unavyoendesha maisha yako. Unaishije? Marafiki zako ni akina nani? Ratiba yako ya kazi ikoje? Nasema hivyo maana kuna mwingine utakuta anaingia kazini saa mbili asubuhi, anatoka saa kumi jioni, basi muda huo yeye ni kuchati na kwenda kukaa baa hadi muda wa kulala.

Kwa utaratibu huo ndugu yangu maendeleo utayasikia kwa wenzako tu. Mtu mwenye uchungu wa maisha na mwenye shauku ya kufanikiwa hawezi kupoteza muda wake kuchati na kukaa baa.

Je, muda huo usingeweza kupata kipato cha ziada kwa kazi yoyote? Kuliko kukaa baa na kupiga soga na marafiki huku ukiteketeza fedha, kwanini muda huo usitumie kuendesha mradi fulani ukakuongezea kipato?

Wengine wanajiuliza, mradi… nitawezaje kuendesha mradi bila mtaji? Ndugu yangu, hivi kutengeneza chapati, bagia au maandalizi – kwa ujumla vitafunwa na ukaviombea dukani asubuhi ukauza, kutahitaji mtaji wa kiasi gani?

Amka usingizini ndugu yangu. Maisha ni wewe tu, kumbuka maisha yako hayawezi kubadilika ikiwa mwenyewe hutabadili namna unavyoishi.

Mada hii itaendelea wiki ijayo katika sehemu ya mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles