31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

YAMOTO BAND JIFUNZENI KUPITIA TMK WANAUME, WANAUME HALISI!

ya moto

Na RAMADHANI MASENGA

YAMOTO Band wako kimya sana kwa sasa. Hii sio kawaida. Wadau wamezoea kusikia nyimbo baada ya nyimbo  kutoka kwao. Yamoto inazua maswali mengi kwa sasa.

Nini kimewapata mpaka wamekuwa kimya hivyo? Wameishiwa? Sio rahisi. Kwa vipaji na shauku wanaoonekana kuwa nayo ni kujidanganya na kuwakosea heshima kusema wameishiwa.

Yamoto Band ni bendi inayoundwa na vijana wenye vipaji halisi. Sasa ni nini chanzo cha ukimya wao? Japo haisemwi ila taarifa zinadai kuna mgogoro unafukuta kati kati yao.

Mgogoro unatajwa kuanza mara tu baada ya Aslay kuoa. Fella anajitahidi kuwaweka sawa ila ni kama inashindikana. Inatajwa kuwa baada ya Aslay kuoa, kuna hali fulani ya kujitenga iliyotokea baina yao.

Kitu hiki kinatajwa kuwa sumu kati yao. Sitapenda kujikita ndani kabisa ya mgogoro wao ila ningependa kuwakumbusha tu hali ya muziki ilivyo.

Hakuna anayebisha kuwa Yamoto ni kundi la vijana wadogo wenye vipaji vikali. Haijawahi kutokea toka watoke wakatoa nyimbo ikabezwa. Kila nyimbo yao ni “hit”.

Ila mbali na hivyo, wanapaswa waelewe umoja wao ndio umewafikisha hapo walipo. Yamoto sio jina la mtu ila ni jina la bendi.

Ladha ya wao watatu ndiyo imefanya watu wawapende na kuwahusudu. Ni ujinga, utoto na uzezeta kwa yeyote kati yao kudhani  kuwa yeye ni bora zaidi kuliko wengine.

Kila mmoja kwa nafasi yake ndiyo kaifikisha Yamoto ilipo. Labda niwakumbushe kitu wadogo zangu wa Yamoto. Kuna kundi lilikuwa linaitwa Gorilla Killers, nao kwa nafasi yao waliwahi kushika chati za juu za muziki nchini.

Kila nyimbo yao ilisubiriwa na wengi na ilipokelewa vizuri. Sijui nini kiliingia katikati yao wakaamua kugawanyika. Kila mmoja akatoa wimbo wake. Nani alizipenda? Wachache.

Mpaka leo hakuna Pingu wala Deso anayetamba kutoka Gorilla Killers. Mara nyingi baadhi ya wasanii walio katika makundi hujidanganya kuwa wao ndiyo chanzo cha kundi fulani kung’aa.  Ni uongo.

Hata B2K wakati inatamba wengi walidhani Omarioni alikuwa analibeba lile kundi. Ila vipi alipotoka, nyimbo zake zilikuwa na umaarufu kama enzi zile alipokuwa katika kundi? Hapana.

Yamoto mna bahati ya kuwa na vipaji vikali huku mkiwa na meneja makini katika duru la muziki. Tulieni wadogo zangu. Kama kweli kuna tofauti kati yenu, fanyeni mzimalize ili muendelee kutimiza ndoto zenu kupitia muziki.

Ujuaji ni moja kati ya mambo yalioua makundi mengi. Mgawanyiko wa TMK Wanaume mpaka Wanaume Halisi uwaonye na kuwafanya mjue hakuna staa katika kundi ikiwa kundi linatamba.

Ujana, umaarufu wa mtaani na ushauri wa wanaojiita wadau usiwafanye mkajisahau na kuona kila mmoja anaweza kusimama kinyake na kuendelea kutamba.

Kila mmoja kwa nafasi yake amheshimu mwenzake. Kama kati yenu kuna kiongozi basi aheshimike na maagizo yake yawe amri. Wasalaam!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles