27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ukawa waja na mpya

Samuel Sitta
Samuel Sitta

NA ELIZABETH MJATTA, DAR ES SALAAM

UTATA mpya umeibuka kuhusu uhalali wa kura zilizowezesha kupatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe wa upande wa Zanzibar, waliopitisha vifungu vya Katiba iliyopendekezwa kupigiwa kura na wananchi.

Utata huo umejitokeza jana baada ya mmoja wa waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka kundi la watu 201, Haji Ambar Khamis, aliyedai jina lake limeandikwa kimakosa katika orodha ya wajumbe wa upande wa Zanzibar walioshiriki na kupendekeza kupitishwa kwa vifungu vya Katiba inayopendekezwa.

Khamis alitoa madai hayo mbele ya waandishi wa habari katika mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia na kufanyika makao makuu ya chama hicho.

Katika madai yake hayo, alisema anaungama mbele ya Watanzania kutoka sakafu ya moyo wake kuwa hakushiriki kwa namna yoyote kupitisha Katiba iliyopendekezwa kinyume kabisa na orodha ya majina yaliyochapishwa ikionyesha jina lake kuwa ni moja ya waliopiga kura za ndiyo.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Khamis alishindwa kuendelea kuzungumzia tukio hilo na badala yake alianza kububujikwa machozi kabla hajachukuliwa kwenda kupumzishwa katika moja ya vyumba vilivyo katika makao makuu ya ofisi hiyo.

Wakati waandishi wakisubiri arejee chumba cha mkutano, alitolewa na kuingizwa katika gari akapelekwa Hospitali ya Amana ambako alifanyiwa vipimo vya moyo wake katika chumba namba 24 kisha alipelekwa kupumzishwa wodi namba tisa.

Wakati Khamis akitoa madai hayo, aliyekuwa Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah alipoulizwa kuhusu hilo, alisema orodha ya wajumbe waliopiga kura ya ndiyo na ile ya hapana bado haijatoka hivyo kuibuliwa kwa tuhuma hizo ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa umakini kwa sababu linaweza kuwa na lengo maalumu.

Dk. Kashililah alisema madai ya Khamis hayana ukweli kwa sababu Katiba inayopendekezwa haitaji majina ya wabunge waliopiga kura ya ndiyo au hapana bali kuna orodha ya walioshiriki kwa namna moja au nyingine kazi za Bunge hilo.

Alisema ripoti kamili ya mwenendo wa Bunge hilo bado inaandaliwa na itatolewa hadharani ikionyesha waliopiga kura ya ndiyo na ile ya hapana.

Awali, kabla ya Khamis kutoa ushuhuda wa jina lake kuingizwa kwa mizengwe katika idadi ya wajumbe waliopiga kura kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Mbatia alielezwa kushangazwa na kile alichokiita mazingaombwe ya kupitisha vifungu vya Katiba.

Mbatia alisema baada ya kupata tetesi za jina la Khamis ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa NCCR–Mageuzi kuwa katika orodha ya wajumbe waliopiga kura ya ndiyo, walianzisha uchunguzi na kubaini kuwa ni la 39 katika ukurasa wa 209 wa Katiba iliyopendekezwa.

Alisema kwa kutambua unyeti wa jambo hilo, Khamis alihojiwa na chama na kukanusha kwa kiapo kushiriki kupiga kura ya ndiyo na kwamba uchunguzi zaidi ulithibitisha kuwa tangu Aprili, mwaka huu baada ya wajumbe wa Ukawa kususia vikao vya Bunge hilo naye hakuwahi kushiriki.

“Mwenzetu alituhakikishia na kuthibitisha kwamba hakuwahi kushiriki katika kuandaa wala kupitisha Katiba hiyo tangu Bunge liliporejea kwa mara ya pili tangu Agosti 5, mwaka huu,” alisema Mbatia.

Mbatia aliituhumu Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo iliyokuwa chini ya Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kwa kueleza kuwa wamefanya ulaghai uliokithiri kwa Watanzania.

Alisema walichokifanya Chenge na Sitta pamoja na wenzao walioshiriki katika ulaghai huo ni udhalilishaji kwa Khamis na familia yake.

Akizungumzia zaidi matokeo ya uchunguzi yaliyofanywa na chama hicho na kuthibitisha kutoshiriki kwa Khamis, Mbatia alisema ilibainika kuwa akaunti yake haikuonyesha kuingiziwa fedha za posho za kuketi katika vikao na malipo mengine waliyokuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge hilo.

Alionya kuwa mwenendo huo wa uchakachuaji katika mambo yanayohusisha uhai wa Taifa ni ishara hatarishi kwa usalama wa nchi.

Aidha, Mbatia alieleza kuwa usalama wa Khamis kwa sasa uko hatarini kwa sababu amekuwa akipokea simu nyingi na ujumbe mfupi kupitia katika simu yake ya kiganjani unaotishia maisha yake na baadhi wakihoji kama alishiriki kweli kupiga kura ya ndiyo.

“Tunajengwa na imani ya hofu kuhusu maisha ya Khamis kwa sababu toka mchakato huu uanze tayari yametokea mauaji ya kikatili na ya kinyama ya mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye ni kiongozi wa chama chetu, Dk. Sengondo Mvungi.

“Pia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama chetu na Kamishna wetu Mkoa wa Mara marehemu Stephen Sebeki ambaye kifo chake kilitokea Julai, mwaka huu, vifo vyote hivi ni vya kutatanisha lakini hakuna majibu yanayoeleweka kutoka vyombo vya dola,” alisema Mbatia.

Nyuma ya pazia

Mtoa taarifa ambaye hakupenda jina lake liandikwe, alilidokeza gazeti hili kuwa taarifa za Khamis kuwindwa na viongozi wa juu wa Bunge hilo zilianza mapema hali iliyowalazimu wenzake kupitia Ukawa upande wa Zanzibar kuanza kufuatilia nyendo zake.

“Kama unakumbuka vizuri kauli ya Sitta kwamba kuna kura mbili upande wa Zanzibar ambazo wanazitegemea, taarifa zilianza kuvuja kwamba Khamis ni miongoni mwa watu wanaowindwa, basi wenzake wa Ukawa walianza kumfuatilia kujua siku ile ya kupiga kura alikuwa wapi, walipowasiliana naye aliwaeleza kuwa yuko Tanga.

“Basi wale wajumbe kesho yake walikwenda hadi Tanga kuzungumza naye juu ya walichokisia, wakiwa Tanga ambayo ndiyo siku ya upigaji kura, walikaa naye hadi kile kipindi cha kupiga kura ambapo jina lake liliitwa Bungeni mara mbili na walijiridhisha kuwa hajapiga kura, sasa hiki kinachotokea ni kwamba hili jambo limetengenezwa kuweza kukidhoofisha chama chetu kwa sababu tayari kimeonekana upande wa Zanzibar kina nguvu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kauli ya Sitta

Akiongoza vikao vya Bunge hilo, Sitta aliwahakikishia wajumbe kuwa baadhi ya wajumbe wanaounda Ukawa wako tayari kupiga kura ya ndiyo kupitisha Katiba inayopendekezwa.

Mwenyekiti  huyo aliliambia Bunge kuwa wajumbe wawili ambao hakuwataja majina kutoka Ukawa wako tayari kupiga kura.

Alidai kuwa mjumbe mmoja kati ya hao ameamua kupiga kura yake na kwamba haogopi kufukuzwa uanachama.

“Mmoja wao yupo tayari kufukuzwa katika chama chake, amepiga kura.

“Maji yanafuata mkondo, jambo ambalo Mungu ameamua haliwezi kuzuiwa na mtu litafanyika tu, huyu mjumbe baada ya kuisoma rasimu iliyopo na kuona manufaa yake ameamua kuipigia kura,” alidai Sitta.

Vimemo vya Sitta

Kwa kile kinachodaiwa kuhakikisha kura ya ndiyo inapatikana, mengi yaliibuka katika Bunge hilo ikiwa taarifa zilizosambazwa zikidai kuwa Sitta aliandika kimemo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuomba wafanye kikao kuhakikisha wanaweka mikakati ya kushawishi baadhi ya wajumbe wa Zanzibar kupiga kura ya ndiyo.

Ujumbe huo ulikuwa ukisomeka kuwa: “Mh. Pinda jaribu kuhakikisha ule mkakati wa kuwapa hela hawa wajumbe watatu maana yake hali sasa ni mbaya hata zile za siri wengi wamepiga HAPANA, naomba tukutane ofisini kwangu, nawajulisha Lukuvi, Wassira na Migiro sasa hivi.”

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles