25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ukawa wafunga kazi

Freeman Mbowe

NA SITTA TUMMA, NZEGA
MWENYEKITI mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe, amesema tayari umoja huo umekwishamaliza kazi katika kupanga safu, kilichobaki ni kusubiri ushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Mbowe aliyasema hayo juzi, alipohutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Taifa, Kata ya Ndala wilayani Nzega mkoani Tabora.
Alisema tayari Ukawa wamekubaliana mambo yote muhimu katika kuelekea kwenye uchaguzi huo na kusema kwa sasa ni vyema vyama vyote vinavyounda umoja huo vikaheshimiana.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, alisema suala la kuheshimiana kwa viongozi na wanachama wa vyama vya Ukawa ni jambo muhimu, na Watanzania wana matumaini makubwa na umoja huo.
Aliwaomba wananchi kutokudanganyika na propaganda za CCM, kwani kuendelea kukichagua chama hicho cha mapinduzi ni laana.
Katika hatua nyingine, Mbowe alishutumu vikali kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kutangaza ratiba ya uandikishaji wapigakura kwa mikoa yote nchini.
Alisema kitendo cha tume hiyo kukaa kimya katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, kinatia shaka na hiyo inaonesha Serikali ya CCM imeingia hofu ya uchaguzi.
Alisema licha ya kubaki miezi mitano kufanyika uchaguzi mkuu, taifa bado lipo kwenye giza nene juu ya hatima ya Watanzania kumchagua rais, wabunge na madiwani.
“Tume hii ya uchaguzi imekuwa ni tume ya CCM, ndiyo maana mpaka leo hii imeshindwa kutangaza ratiba ya uandikishaji wapigakura katika mikoa mingine nchini.
Hata kuandikisha wapigakura huko njombe kwa kutumia bvr ni usanii mtupu. hii ni hofu ya uchaguzi ambapo CCM na Serikali yake inahofia kuangushwa na ukawa mwaka huu,” alisema mbowe na kushangiliwa.
“Ukiona taifa lenye kundi kubwa la vijana masikini wasiokuwa na ajira, elewa nchi hiyo inamatatizo makubwa ya kiutawala.
“Serikali ya Ukawa, inakwenda kujenga taifa lenye nidhamu kwa viongozi, kukomesha wizi na ufisadi, kulinda mali zote za umma na kujenga uchumi imara, viwanda na ajira kwa wananchi wake,” alisema.
Apuuza agizo la IGP
Jana akiwa wilayani Itilima mkoani Simiyu, Mbowe alipuuza amri iliyotolewa juzi na Mkuu wa Polisi (IGP), Ernest Mangu ya kupiga marufuku vyama vya siasa kuunda vikundi vya ulinzi.
Alisema Chadema haitatii amri hiyo na ni heri wauawe kuliko kuacha kutoa mafunzo ya maadili na kizalendo kwa vijana katika taifa lao masikini.
Mbowe ambaye jana alisimikwa na kupewa vifaa vya utemi wa kabila la wasukuma na kupewa jina la Mayengo, aliyasema hayo alipokuwa akihutubia halaiki ya wananchi alipokuwa akifunga kambi ya vijana wa Chadema eneo la Lagangabilili wilayani Itilima.
Alisema viwango vya kimataifa juu ya ulinzi wa raia askari mmoja anapaswa ahudumie wananchi 140, nchini askari mmoja anahudumia watu 3,000.
“Katiba yetu ya nchi inatambua haki ya mtu kuishi, hivyo lazima tujilinde bila kusubili ulinzi wa polisi ambao ni wachache.
“Namtaka IGP Mangu afahamu kwamba Polisi hao hao wanaomba jamii ishiriki ulinzi shirikishi,halafu polisi hao hao wanataka kuzuia vijana kupewa mafunzo ya kukabiliana na uhalifu, hatutakubali ni heri watuuwe,” alisema.
Hata hivyo, Mbowe alimwonya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuacha kuviingilia vyama katika mambo yake yaliyomo katika katiba za vyama vyao.
Bila kutaja mambo yanayoingiliwa na Jaji Mutungi, Mbowe alisema: “Kama huyu Mutungi anataka kufanya siasa avae shati la kijani na apande majukwaani ili chadema tumwoneshe kazi. Nasema hii ni rasharasha tu bado kazi,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare alisema mafunzo wanayopewa vijana wa Chadema ni ya kizalendo kwa ajili ya kulinda kura, mali za umma, ukakamavu na afya.
Alisema ni aibu kwa Jeshi la Polisi kukataa kutoa mafunzo ya kupambana na uhalifu kwa vijana waliokuwa kwenye kambi hizo za Chadema.
“Mheshimiwa Mwenyekiti Mbowe, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wao wanakuja kutoa mafunzo kwa vijana wetu namna ya kupambana na rushwa, lakini Polisi wao wamekataa. Kwa vile wewe unaongea na waziri wao, Waziri Mkuu na rais, nakuomba ukawashtaki Polisi hawa,” alisema Lwakatare.
Aliwaomba vijana na wananchi wote kulinda kura wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, ili kudhibiti wizi wa kura za wabunge, madiwani na rais.
Mbowe ateta na Maalim Seif
Katika hatua nyingine, habari za uhakika ambazo MTANZANIA imepata zinasema wiki iliyopita Mbowe alikutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na kufanya naye mazungumzo ya siri kwa saa mbili.
Chanzo chetu cha habari kinaeleza kuwa, katika mazungumzo hayo, Chadema iliomba iachiwe majimbo 15 Zanzibar.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Maalim Seif alikubaliana na ombi hilo kwa sharti kuwa Chadema isimamishe wagombea katika majimbo ya Unguja ili kumaliza nguvu ya CCM na CUF ibaki na ngome yake ya Pemba.
Chanzo hicho kilieleza kuwa mazungumzo hayo bado hayajafikiwa mwisho, ingawa Maalim Seif anaonekana kuwa yupo tayari kutoa majimbo 10 ya Unguja.
“Katika majimbo hayo, yamo yanayoshikiliwa na CCM lengo ni kuongeza ushindani, kwa sasa Unguja na Pemba kuna majimbo 50. Pemba inamajimbo 18 na Unguja 32,” kilisema chanzo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles