25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa: Lowassa anaongoza

MMGL1140VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimetoa matokeo ya utafiti uliofanywa sehemu tatu tofauti unaoonyesha mgombea wao wa urais, Edward Lowassa, atapata ushindi wa asilimia 76.

Matokeo ya utafiti huo yalitolewa   Dar es Salaam jana ikiwa ni siku chache tangu   Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza itoe utafiti wake ambao ulimpa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ushindi wa asilimia 65 na Lowassa ushindi wa asilimia 25.

Kabla ya Twaweza,  Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia kilitoa utafiti wake uliompa    Dk.   Magufuli ushindi wa asilimia 69.

Akitoa ripoti ya utafiti huo jana, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema Ukawa umefanya utafiti mara tatu ambao ulishirikisha watafiti wa ndani, nje na kwa njia ya mitandao.

“Utafiti uliofanywa na watafiti wa ndani umeonesha kwamba Lowassa atapata ushindi wa asilimia 76, watafiti wa nje wameonesha atapata asilimia 74 huku wale wa mitandao ya simu na kompyuta wamekipa Ukawa ushindi wa asilimia 79,” alisema.

Mbatia alisema licha ya Ukawa kuwa na utafiti huo ambao umefanywa na watu makini,  i wameendelea kuwa kimya bila ya kutangaza hadharani kama wanavyofanya wengine.

“Hivyo natoa wito kwa wapiga kura kuzipuuza takwimzilizotolewa na Twaweza ambao kwa sasa nawaita ‘Twabagua’, kuwa zinalenga kuibeba CCM,” alisema Mbatia.

Baregu aikosoa Twaweza

Naye Mjumbe wa jopo la Ukawa, Profesa Mwesiga Baregu alisema utafiti wa Twaweza unaonesha udhaifu mkubwa kwa vile  umechelewa kutolewa tangu ulipofanyika.

“Ili utafiti uwe mzuri lazima matokeo yatolewe mapema kwa sababu kila muda unapopita mambo hubadilika na kama ukichelewa husababisha taarifa kuwa mfu… na nadhani hicho ndicho kilichotokea kwa Twaweza,” alisema Profesa Baregu.

Alisema utafiti wa Taweza ulifanyika Agosti kabla ya wagombea hawajachukua fomu hivyo ulipaswa kutolewa muda huo na si hivi sasa mwishoni mwa Septemba.

Profesa Baregu alisema upungufu mwingine uliofanywa na taasisi hiyo   ni kuwatumia watafiti hao hao kwa muda mrefu bila kuwabadilisha jambo linaloweza kuharibu utafiti kwa kutoa majibu yanayomfurahisha muulizaji.

Alisema watafiti waliotumiwa na Twaweza wamekaa na simu za kufanyia utafiti kwa mkataba wa miaka mitatu ambao ndiyo wengi na wengine miezi sita, hali ambayo haiwezi kutoa takwimu sahihi na zisizokuwa na upendeleo.

“Twaweza walitakiwa kupiga simu kwa watu tofauti tofauti bila ya kuwaandaa kwa kuwapa simu. Wangeshirikiana na kampuni za simu kupiga na kuuliza moja kwa moja  maswali ingeweza kuwasaidia kupata utafiti mzuri,” alisema Profesa Baregu.

Kwa upande wake Mbatia alisema utafiti wa Twaweza una kasoro za utafiti  kwa vile waliotafitiwa walipewa bure simu na vifaa vya kuongeza nguvu (charger),  vinavyotumia mwanga wa jua.

Alisema utafiti wa Twaweza unasema taarifa inawakilisha maoni ya wananchi kuhusu siasa mwaka 2015, lakini inaishia kuwalinganisha wagombea wa Ukawa na  CCM huku wagombea wengine sita hawapatiwi umuhimu unaotakiwa.

“Pamoja na kudai kwamba utafiti huo ni wa kitaifa lakini wameshindwa kuiwakilisha sehemu moja ya Muungano ambayo ni Zanzibar katika utafiti huo,” alisema Mbatia.

Kasoro nyingine iliyoelezwa na Mbatia ni suala la watafiti kutofahamu maana ya Ukawa kwa kusema kuwa ni walinzi wa Katiba ya wananchi.

Mbatia alisema walishindwa kuthamini kwa usawa michango ya vyama vya ADC, Chaumma, NLD, NRA, UPDP na TLP kwa kutoviwekea takwimu za moja kwa moja na kuvijumuisha pamoja kwa kuviita ‘vingine’.

Aliitaja kasoro nyingine kuwa ni kitendo cha kuorodhesha vyama visivyokuwa na wagombea urais katika swali la kuchagua rais, kwa mfano CUF na NCCR –Mageuzi.

Alisema kuwa majumuisho ya matokeo ya utafiti hayaendani na maswali ya utafiti, kwa mfano swali lilikuwa ‘uchaguzi ungefanyika leo ungemchagua mgombea wa chama gani?.

“Cha kushangaza   hitimisho lake lilikuwa ni kwamba CCM ndicho chama kinachopendwa zaidi na wanaokiunga mkono Chadema wamepungua tangu 2013!” alisema Mbatia.

Mbatia aliitaka Twaweza iache kutumiwa na CCM kwa sababu ni taasisi inayoheshimika kwa kudhamini na kuthamini midahalo inayohusiana na Uchaguzi Mkuu.

Alisema   kwa sasa Ukawa inawaalika Twaweza katika mdahalo wa wataalamu waliobobea katika takwimu na wawakilishi mmoja mmoja wa kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi mkuu ili taasisi hiyo itetee taarifa yake.

Mdahalo

Akizungumzia   suala la mgombea urais wa Ukawa kushiriki kwenye midahalo, alisema wapo tayari kushiri mdahalo utakaoitishwa na taasisi yoyote lakini kwa masharti kuwa kabla ya kufanyika wakae  meza moja,   vyama na waandaaji ili kujadiliana utaratibu wake.

Kuhusu suala la Lowassa kupewa mwaliko wa kushiriki mdahalo na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mbatia alisema hajaiona barua hiyo katika ofisi za vyama vinavyounda Ukawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles