* Wapigwa marufuku kula, kunywa wakati wa kuaga
*Lowassa, Mbowe na Sumaye kuongoza waombolezaji
NA BENJAMIN MASESE, MWANZA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela imetoa saa tano kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutumia Uwanja wa Furahisha kwa ajili ya kuaga mwili wa marehemu Alphonce Mawazo, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Akitoa ratiba mpya ya kuaga mwili wa Mawazo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Geita mjini hapa jana, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, alisema shughuli hiyo itafanyika katika uwanja huo na kuhudhuriwa na wabunge wa vyama vinavyoundwa Ukawa na watajitahidi kuzingatia maelekezo hayo ili watoe heshima zote zinazostahili.
Pia alisema shughuli hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
“Kiongozi mkuu atakayeongoza shughuli za kuaga mwili wa Mawazo atakuwa Mbowe, lakini katika shughuli hiyo kutakuwa na viongozi wa kitaifa ambao ni aliyekuwa mgombea nafasi ya urais kupitia Chadema, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wabunge wa Ukawa na watu wengine maarufu.
“Sasa kutokana na kupewa saa tano za kutumia uwanja huo, tutakuwa na makundi maalumu ya watu katika kupewa nafasi ya kuzungumza ili kuwawakilisha wengine, tunaomba wananchi watakaohudhuria pale waepuka kula chakula ovyo au kunywa, isije ikatokea mmoja akatapika, kuugua tumbo wakasingizia mkusanyiko wetu.
“Tambueni tulikuwa tumepewa saa tatu, ikabidi tuzungumze na Mkurugenzi wa Ilemela, John Wanga, ili kuongeza muda, natumia nafasi hii kuwataarifu Watanzania kwa ujumla kuwa Mawazo ataagwa kwa awamu nne, tunaaga hapa Mwanza kama kitaifa, kisha Geita Mjini sehemu ya mkoa aliokuwa akiongoza.
“Pia tutaaga Katoro kama sehemu ya Jimbo la Busanda alilogombea ubunge na mwisho atazikwa kijijini kwao Chikobe Jumatatu ya Novemba 30, mwaka huu, ambapo wananchi wa pale watapewa nafasi ya kumuaga,” alisema Mwalimu.
Kwa mujibu wa ratiba aliyoisoma, inaonyesha mwili wa Mawazo utaondolewa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza leo kati ya saa 2:30 – 3:00 asubuhi na kupelekwa nyumbani kwa Mchungaji Charles Lugiko, ambaye ni baba yake mdogo eneo la Nyagezi-Sweya na utaagwa kwa taratibu za mila na desturi.
Pia ratiba hiyo iliyonyesha kuwa kati ya saa tano asubuhi hadi saa sita mchana, mwili wa Mawazo utakuwa njiani kuelekea Uwanja wa Furahisha kwa ajili ya kuagwa kitaifa na inakadiriwa kufanyika kuanzia saa 6:30 hadi saa 8:00 mchana kabla ya kuanza safari ya kwenda Geita Mjini na waombolezaji watalazimika kulala hapo.
Ratiba hiyo inaendelea kuonyesha kuwa kesho asubuhi mwili wa Mawazo utaagwa tena Geita Mjini katika Uwanja wa Magereza, kabla ya kusafirishwa hadi Katoro ambako utaagwa tena kama sehemu ya jimbo lake na baadaye kuupeleka kijijini kwao Chikobe na mazishi keshokutwa asubuhi.
Katika hatua nyingine, Mwalimu alitoa shukrani kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, kupokea hukumu bila kinyongo na kuahidi kutoa ushirikiano katika ulinzi wakati wa shughuli za kuaga na kusafirisha mwili huo.
Alisema tayari baadhi ya viongozi wa Chadema wametangulia mkoani Geita kwa ajili ya kuonana na polisi ili kupanga namna ya kufanikisha shughuli hiyo.
Mawazo aliuawa Novemba 14, mwaka huu mkoani Geita na watu wasiojulikana baada ya kumvamia akiwa njiani na kumkata kwa mapanga na shoka na kusababisha kifo chake.