27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UKATILI UNAWEZA KUMFANYA KUONEKANA SHUJAA  

 

Na CHRISTIAN BWAYA


HUENDA unamfahamu mtu aliyewahi kufanya kitendo cha ukatili kiasi cha kukuacha mdomo wazi. Inawezakana ulimfahamu mtu huyo kama muungwana, mpole, mnyenyekevu na mpenda watu lakini hukuamini ni yeye huyo huyo anaweza kumsababishia maumivu makali mtu mwingine.

Matukio kama hayo hutufanya tukahisi huenda watu hawa walikuwa na ukatili wa kichini chini ndani yao ingawa mazingira hayakuruhusu asili hiyo ya ukatili kuonekana. Kama tulivyoeleza katika makala iliyopita, hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa ukatili ni tabia ya kuzaliwa nayo kama watu wengi wanavyoamini.

Tunafahamu kuwa mazingira yanaweza kukufanya kuwa mtu mwingine. Fikiria umevamiwa na mtu anayehatarisha uhai wako. Katika mazingira kama haya, ni wazi utajitetea kwa kufanya kitendo ambacho usingeweza kukifanya ukiwa katika hali ya kawaida. Maana yake ni kwamba tabia zetu hugeuka kukidhi mahitaji ya mazingira tunayokuwapo.

Tuliona utafiti wa mwanasaikolojia Stanley Milgram aliyataka kujua mazingira gani huchochea ukatili ndani ya mtu. Lililo wazi katika utafiti wake ni kwamba kila mtu kwa wakati wake anaweza kuwa mtu katili na kumsababishia maumivu makali na hata kuutoa uhai wa mtu mwingine. Katika utafiti wake tulioueleza katika makala yaliyopita, watu sita kati ya 10 walikuwa tayari kuongeza adhabu iliyotosha kumuua mwanafunzi wao! Milgram alishangazwa.

Hata hivyo, aligundua kwamba watu hufanya vitendo vya ukatili kama huo kwa nia njema kabisa. Jambo hili linashangaza kidogo kwa sababu huwa tunaamini mtu anayemuumiza mwenzie, anafanya hivyo kwa sababu anafurahia kuona mwenzake akiumia. Tukirejea utafiti wa Milgram, washiriki wale walifanya kitendo cha ukatili wakati wao wenyewe wakiumia kwa kufanya walichokuwa wakikifanya.

Kumbe shinikizo la kufanya ukatili lilitoka kwa mtafiti ambaye kama tulivyoona, aliweka mazingira ya kuheshimiwa kwa namna isiyokubalika. Kila wakati mshiriki alipofikiri kuacha, shauri ya kusutwa na nafsi, alikumbushwa na mtafiti kuwa hicho anachokifanya kilikuwa sahihi na kwamba anayewajibika na kitakachotokea ni yeye mtafiti.

Mamlaka aliyokuwa nayo mtafiti yalimfanya mshiriki afanye kitu asichokifurahia kwa sababu tu hakuwa na nguvu ya kusimamia dhamira yake. Nidhamu, heshima na utii kwa mtafiti aliyejitambulisha kama Profesa wa Chuo Kikuu, vilimfanya mshiriki ajikute hana namna nyingine isipokuwa kutii.

Kimsingi, Milgram anatuambia ukatili ni tabia ya kimfumo zaidi kuliko hiari ya mtu. Ukatili unatengenezwa na mfumo na kisha hubisha hodi kwa mtu mmoja mmoja. Jamii inapoanza kukubali tabia ya matumizi ya nguvu na kuyachukulia kama hali ya kawaida, hali hiyo hutengeneza shinikizo la ukatili ndani ya watu.

Fikiria watu waliozoea kudai haki kwa kushikana mashati. Fikiria mazingira ambayo hoja na mantiki havina nafasi ya kukupa kile unachoamini unastahili. Mazingira kama haya hutengeneza shinikizo la mtu mmoja moja kuitafuta haki hiyo kwa kumwuumiza mtu mwingine ‘kwa nia njema.’

Lakini jambo la pili, ni kwamba wakati mwingine watu hufanya ukatili kama namna ya kujihakikisha mamlaka. Bahati mbaya ni kwamba kila mwanadamu ana kiu na njaa ya kuwa na mamlaka. Inawezekana ikawa ni mamlaka dhidi ya watu wengine, au ushawishi kwa wanaohisiwa kuwa na mamlaka.

Kama ilivyokuwa kwa walimu wa utafiti wa Milgram waliokuwa wanafanya wasichokiamini kama ishara ya utii, ndivyo na sisi kama binadamu tunavyoweza kuwa na utayari wa kumtii mtu tunayeamini anayo mamlaka kwa kuwaumiza wengine. Tunafahamu wapo vijana wahalifu hulazimika kufanya vitendo vya ukatili kwa wengine kwa lengo la kumfurahisha mkubwa wao.

Kadhalika, mwanadamu ana hulka ya kutaka kuonekana shujaa dhidi ya wengine. Shujaa ni mtu anayesifika kwa kufanya kitu ambacho watu wengine hawajakifanya. Utakumbuka simulizi ya Daudi aliyejipatia umaarufu kwa kumuua adui wa taifa lake aitwaye Goliathi. Hatua hiyo ilimtengenezea umaarufu katika jamii ya wana wa Israel.

Hata hivyo, ushujaa huo wa Daudi ulitishia ushujaa wa mfalme Sauli ambaye naye alitamani kuwa maarufu. Shauku ya kutaka kuwa shujaa, ilimfanya Sauli awe mtu mwingine. Mbali ya kuwa na ghadhabu kubwa dhidi ya Daudi aliyeanza kumchukulia kama adui yake, Sauli alianza kupanga mipango ya kummaliza mbaya wake aliyekuwa anatishia ushujaa wake.

Ni vyema kuwa makini pale unapokuwa na shauku kubwa ya kuonekana shujaa. Hali hiyo, kisaikolojia ni kichocheo kikubwa cha matendo yanayoweza kuwaumiza watu watakaotishia shauku hiyo. Pamoja na hulka ya kutamani kuwa watu watakaokumbukwa kwa kufanya mambo fulani katika jamii, lazima kuwa na ‘gavana’ ikusaidie kujizuia kuvuka mipaka.

 

ITAENDELEA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles