UNa JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM
UKATA umekuwa kama jambo la kawaida kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara hapa nyumbani, lakini wakati mwingine mambo hayo ni ya kujitakia.
Ufike wakati klabu zijiwekee mipango sahihi na njia salama za kujiingizia kipato ili kujiendesha na kuhakikisha zinashiriki vema mechi zote za ligi.
Suala la klabu kushindwa kujiendesha na kujikuta wachezaji wakidai mishahara, limekuwa likionyesha picha mbaya kwa wadau wa soka na hata wasimamizi wakuu wa soka ambao ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Klabu kushiriki ligi ikiwa inasuasua kwenye mambo mbalimbali, daima haitaweza kupata matokeo bora yenye afya, si matokeo ya uwanjani tu, hata wachezaji wenyewe watashindwa kuendeleza vipaji vyao.
Umefika wakati viongozi wa kila klabu kuamka, kuumiza vichwa vyao na kujua pindi wanapopewa jukumu la kuendesha na kusimamia timu, lazima wazingatie vyanzo vya kujiingizia mapato.
Tunahitaji kutoka hapa tulipo, tunahitaji kuwa na timu zenye kiwango bora na uwezo mzuri ndani na nje, hivi vyote haviwezi kupatikana ikiwa klabu zinajiendesha kwa kusuasua.
Tunapaswa kubadilika tujifunze kupitia nchi za wenzetu ambazo ligi zao zimekuwa zikiendeshwa kwa ushindani zaidi na kila timu imejiwekea mipango endelevu ya kujikusanyia kipato.
Licha ya kuonyesha kiwango kibovu, ni mara chache sana utasikia timu imeshindwa kujiendesha kwa kukosa fedha au kutokuwa na wadhamini wanaoeleweka.
Lakini kwa hapa nyumbani ni kama wimbo ambao umekuwa ukijirudia masikioni mwa wasikilizaji kila baada ya msimu, kwani lazima suala la ukata lijitokeze.
Daima tunaendelea kushuhudia nchi za wenzetu zikipiga hatua sisi tutaishia hapa, mchezaji akitoka kwenye timu yenye hali duni na kusajiliwa Simba, Yanga, anaona amekamilisha malengo yake.
Tunahitaji kuzalisha vipaji na kumiliki wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, kwa staili hii hatutaweza kufanikiwa kwani tayari wachezaji wamejikatia tamaa, jambo linalopelekea wengine kufanya migomo baridi.
Hatuwezi namaanisha tusipojitoa hapa tulipo, tutashuhudia maendeleo kwa wenzetu tu, msingi bora wa mchezaji hujengwa na klabu bora inayojali masilahi yake.