23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TFF iwe macho lala salama Ligi Kuu Bara

TLIGI Kuu Tanzania Bara inazidi kuelekea ukingoni, huku vita kubwa ikionekana kwa timu zinazopigania kutoshuka daraja.

Takribani timu 12 au 13 zipo katika hatari ya kushuka daraja, ambapo yoyote itakayofanya makosa kwenye mechi zake zilizobaki, inaweza kujikuta ikirejea Ligi Daraja la Kwanza.

Timu hizo ni African Lyon, Biashara United, Singida United, Kagera Sugar, Ndanda FC, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Stand United, Mwadui, Mbeya City, Ruvu Shooting, Coastal Union na JKT Tanzania ambazo pointi zao ni kati ya 21 na 35.

Kwa jinsi hali ilivyo, timu iliyopo mkiani ni African Lyon, iwapo itashinda mechi 10 kati ta 18 zilizobaki, inaweza kufikisha pointi 51, ikiwa ni pointi 16 zaidi ya 35 walizonazo JKT Tanzania iliyopo nafasi ya nane.  

Kutokana na hali hiyo, ni wazi timu zote hizo hazitatakiwa kufanya makosa katika mechi zao zijazo, hali inayoweza kusababisha viongozi kutumia kila njia ili ziweze kuvuna pointi na kubaki Ligi Kuu Bara.

Kwa hali kama hiyo, ni wazi kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linatakiwa kuwa makini kuhakikisha hakuna rafu zozote zinazoweza kuchezwa ili kuziwezesha baadhi ya timu kushinda ‘nje ya uwanja’.

Uzoefu unaonyesha mara nyingi dakika za lala salama za ligi hiyo, huambatana na matukio kadha wa kadha ya udanganyifu wa matokeo ili kuzibeba timu zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja kama ilivyo kwa zile zinazopigania ubingwa.

Na kwa kuwa waamuzi ndio wenye jukumu la kutafsiri sheria zote 17 zinazoongoza mchezo wa soka, hivyo basi ni vema TFF kwa kushirikiana na Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT) na Kamati ya Waamuzi, kuwafuatilia kwa karibu marefa kuhakikisha hakuna anayerubuniwa ili kuibeba timu fulani.

Kila timu ni vema ikajituma kadiri ya uwezo wao ili kupata matokeo kulingana na uwezo wao na si vinginevyo.

Lakini pia, umakini huo wa waamuzi uelekezwe pia kwa upande wa timu zinazowania ubingwa, huku nafasi kubwa ikionekana kuwa kwa vinara wa ligi hiyo, Yanga, mabingwa watetezi Simba na hata Azam.

Waamuzi ni vema wakawa makini na kujiepusha na udanganyifu wa matokeo ili kuendelea kulinda heshima yao mbele ya wadau wa soka hapa nchini.

Lakini pia, wachezaji na viongozi kila mmoja awajibike kadiri ya uwezo na nafasi yake ili kuzisaidia timu zao kupata ushindi badala ya kutegemea mbeleko ya waamuzi. 

Ni kwa kufanya hivyo, mwisho wa siku Tanzania Bara itampata bingwa halali, lakini pia timu zitakazoepuka wimbi la kushuka daraja zitakuwa ni zile zilizostahili.

Ikumbukwe kuwa udanganyifu wa matokeo umekuwa ukichangia soka la Tanzania kudorora na mwisho wa siku, timu zetu zikiishia kuwa wasindikizaji kwenye michuano ya kimataifa.

Kazi kwenu waamuzi wa Ligi Kuu Bara, chonde chonde, tendeni haki kwa kufuata sheria zote 17 za soka ili kuwatendea haki wadau wa mchezo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles