Serikali imesema itaendelea kuwakamata wamiliki na madanguro, wanawake wanaojiuza na wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wazee, Dk.Hamisi Kigwangallah amesema hayo bungeni leo na kuongeza kuwa mwanamke anayeishi akitegemea kipato kutokana na ukahaba ni kosa kisheria hivyo nao watakamatwa.
Dk. Kigwangallah alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Geita Vijijini, John Kanyasu (CCM), aliyetaka kujua agizo la kuwakamata wanawake wanaojiuza kama linafanyiwa kazi.
“Kwa mujibu wa vifungu vya sheria namba 146 (a) na 176 (a) vya sheria ya makosa ya jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa.
“Katika kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo viongozi katika mikoa mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Dar es salaam, wamewachukulia hatua wanawake wanaojiuza,” amesema Dk. Kigwangallah.
Hata hivyo, Dk. Kigwangallah alisema mikoa inayoongoza kwa makahaba kujiuza ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.