26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UKABILA KWANZA, UTAIFA BAADAYE

Na MARKUS MPANGALA

AGHALABU mjadala ukipamba moto juu ya Katiba mpya na siasa za Kenya. Sehemu inayosifiwa ni uhuru wao katika masuala mbalimbali ya kisheria na taratibu za kuongoza nchi.

Kenya wanasifiwa kutokana na Mahakama kutengua matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.  Jaji Mkuu David Maraga pamoja na wengine watatu walikubali uchaguzi urudiwe, huku wawili wakipinga.

Sasa uchaguzi wa Kenya umerudiwa. Kwa msingi huo inasifiwa katiba na kulaumiwa tume ya uchaguzi. Tuanzie hapo, inaitwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Ninaamini huo ni urembo wa kisiasa ambao hutumiwa kama kichaka cha kuficha udhaifu mwingine. Udhaifu wa kwanza wa Kenya ni siasa za kikabila. Muundo wa siasa zao haufanani na siasa za Tanzania wala Uganda.

Siasa za kutazama kabila kwanza zimetamalaki katika nchi za Sudan Kusini, Burundi, Rwanda na Kenya. lakini mwenendo huo wa kisiasa umekuwa sehemu ya maisha yao kwa miaka mingi sana.

Makabila yenye nguvu na idadi kubwa ya watu ni Wakikuyu na Kalenjing. Makabila hayo ndipo anakotoka Uhuru Kenyatta (Mkikuyu) na naibu wake William Ruto (Mkalenjing).

Uchaguzi wa mwaka 2013 nilikuwa naongea na rafiki yangu mwanahabari na mwalimu raia wa Kenya, Dorine Otinga, ambaye alikuwa miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi huo. Mara kwa mara alisisitiza kuwa kama hakuna maridhiano kati ya Wakalenjing na Wakikuyu kisiasa mambo yanakuwa mabaya zaidi.

Aliniambia ili kuendesha siasa kwa Kenya suala la ukabila ni jambo la kisiasa. Ni kama falsafa yao ya kisiasa (Political Ideology). Kwa hiyo urembo wa maneno ya “Tume Huru na Mipaka” kuelezea Tume ya uchaguzi halikuwa suluhisho la mambo. Ilikuwa sawa na kuweka urembo tu katika sehemu ambayo wenyewe wanaficha uhalisi wa tabia zao kisiasa. Yote yamedhihirika katika uchaguzi wa marudio.

Mfano ni kampeni iliyoanzishwa na mshauri wa kampeni na mratibu wa Raila Odinga na Nasa, David Ndii. Mwanazuoni huyo alikuwa akisisitiza juu ya kuanzishwa “Kenya mbili”. Dhumuni lake lilikuwa kuonyesha kwamba Kenya inatakiwa kutawaliwa kwa misingi ya maelewano ya makabila.

Mchumi huyo alisisitiza Kenya igawanywe kwa misingi ya kikabila. Pia Nasa pia wanataka kuonyesha ulimwengu kwamba ni upinzani jasiri tu unaoweza kukabiliana na vitisho vilivyojaribu kusakama mashirika yasiyokuwa ya kiserikali dhidi ya kwenda kortini.

Mwanazuoni huyo  alitoa pendekezo hilo Agosti 22, mwaka huu wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha NTV katika kipindi cha “Decesion2017”. Ndii alibainisha kwamba Kenya ina jumla ya makabila 44, ambapo kwa kipindi cha miaka 50 tangu walipopata uhuru wao wameongozwa na makabila mawili tu; Wakikuyu na Kalenjing.

Kwa mujibu wa Ndii ambaye alipendekeza sehemu ya kwanza itaitwa “Central Republic of Kenya” wakati sehemu ya pili itaitwa “People’s Republic of Kenya”. Ikiwa na maana kwamba Kenya igawanywe kama ilivyokuwa Sudan ambako kumetengenezwa mataifa mawili yaani Sudan na Sudan Kusini.

Mgawanyo wao uwe hivi; Western Kenya; ukanda huo uundwe na maeneo ya Luo, Luhya, Teso, Kisii na Kurial. Halafu upande wa Coastal Kenya; uwe na maeneo ya Swahili, Mijikenda, Pokomos, Giriamas, Taifa na Taveta. North West Kenya itaundwa na maeneo ya Turkana na Pokot.

Kukamilisha hatua hiyo alitangaza kufungua shauri au madai katika Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika (African Commision on Human and People’s Right) yenye makao yake mjini Banjul nchini Gambia. Sababu kubwa aliyotaja ni kutokana na maelezo kwamba, kulingana na Tume hiyo wananchi wanao uhuru kulinda haki zao za kujitawala pamoja na kuanzisha taifa lao bila vikwazo vyovyote.

Wafuasi wanaotaka Kenya igawanywe wanaegemea katika Ibara ya 10 ya Mkataba wa Banjul (Banjul Charter) kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, inasema, “Watu wote watakuwa na haki ya kuishi na kutawala, watakuwa huru kuamua mwelekeo wao wa hadhi ya kisiasa na watakuwa huru kutekeleza sera zao za uchumi na maendeleo ya jamii kwa mujibu wa kanuni na taratibu walizozichagua kwa uhuru wao.”

Aidha, nimeshuhudia mjadala mzito katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo baadhi ya Wakenya walihoji kwanini nchi yao imetawaliwa na makabila mawili pekee.

Jambo hilo linanisukuma kuamini kuwa suala la kabila lako nchini Kenya ni la kwanza kisha unafuata utaifa. Kwa hiyo linapokuja suala la watu kwenye farashani zao wakisema Kenya inatufundisha mengi, inatupasa pia kufahamu pia hasara yake.

Mathalani, kufutwa matokeo ya urais kulipambwa kwa namna nyingi. Tume ya uchaguzi inalalamikiwa kukiuka sheria za uchaguzi na katiba ya nchi yao. Wengine wanasema kulikuwa na wizi wa kura ambazo hazikuelezeka. Mahakama ya Juu walisema baadhi ya kura 11,000 hazikuhesabiwa.

Katika imani yangu ya dini tunaagizwa kumbushaneni. Kwamba katika kukumbushana kuna salama itashuka. Hapo ndipo ninapotazama Kenya kwa jicho jingine, kuanzia uchaguzi, kampeni ya Kenya mbili ya David Ndii hadi hukumu ya Mahakama utabaini jambo moja tu; kabila lako ni muhimu.

Endapo Wakenya wangewekeza nguvu kutafuta njia ya kutibu mpasuko wa kikabila, wasingeendelea kuuana mara kwa mara. Lakini kwa kuwa waliona katiba ndilo tatizo wamejikuta hawajatatua tatizo la msingi linalowakabili. Kama nilivyosema awali, tume ya uchaguzi ilirembwa tu kujifurahisha mwonekano ilhali tatizo la msingi halikutatuliwa.

Tumeshuhudia mivutano ya kisiasa yenye “Nembo” ya Wakamba (Kalonzo Musyoka) na Wajaluo (Raila Odinga) kwa upande mmoja dhidi ya Wakikuyu (Kenyatta), Kalenjing (Ruto) na Wamasai. Kwamba Wajaluo na Wakamba wanaamini makabila ya Wakikuyu, Wakalenjing na Wamasai ndio chanzo cha  tatizo. Na makabila mengine yanawatazama Wajaluo na Wakamba vivyo hivyo.

Nchi ya hivi hata hata wafanyeje na kuiremba Katiba yao watakabiliana na jinamizi hilo kila waendako. Ni nchi ambayo inakubali kuona kabila ndicho kitu cha kwanza katika uchaguzi wao, itaendelea kuumizwa kama ilivyokuwa Sudan Kusini ya sasa. Haipendezi lakini inatia kinyaa mno pale makabila yanapochukua nafasi zetu za utaifa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles