CWT KUMBURUZA KORTINI DC ALIYEWAPIGISHA WALIMU ‘PUSHAPU’

0
717

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kinakusudia kumburuza mahakamani aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Gelasius Byakanwa baada ya kugoma kuwaomba radhi dhidi ya madai ya kuwadhalilisha walimu ikiwamo kuwapigisha pushapu.

Mwenyekiti wa CWT wilayani humo, Joseph Maimu amesema kusudio la kufungua kesi ya udhalilishaji dhidi ya Mkuu huyo wa Wilaya ambaye sasa amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, linaendelea kukamilishwa na wataalamu.

“Tumekwishaandaa mwanasheria kwa hatua za awali za kufungua kesi dhidi ya Mkuu wa Wilaya, tumechukua uamuzi huu baada ya yeye kutoona umuhimu wa kutafuta suluhu ya matatizo yaliyotokea wakati wa ziara ya kutembelea shule za Sekondari wilayani mwetu,” amesema.

Awali akisoma tamko la CWT, Katibu wa chama hicho, Anisia Lyimo amesema kitendo alichokifanya Byakanwa hakikuwa cha kiungwana wala kutambua thamani ya walimu na taaluma kwa ujumla.

“Sisi waalimu wilayani Hai tunatambua kuwa Mkuu wa Wilaya ni mwakilishi wa Rais katika wilaya husika. Lakini vitendo vilivyofanywa na Byakanwa dhidi ya walimu vinaonyesha jinsi mkuu huyo alivyowadharu walimu, tulimpa siku 30 za kutafakari na kutafuta usuluhishi wa tatizo, japokuwa hadi leo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameendelea kutoona umuhimu wa kutafuta usuluhishi,”alisema.

Kwa upande wake Byakanwa akizungumzia madai hayo ya walimu alisema, hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwani CWT hakijamtafuta.

Mkuu huyo wa wilaya wa zamani, anadaiwa kuwadhalilisha walimu kwa kuwaamuru wapige  pushap, kuwaweka mahabusu kwa saa sita huku akiwaita vilaza na kumkemea Mwalimu Mkuu na kumueleza kuwa hana nidhamu mbele, ya walimu wenzake.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here