25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

UJINGA WA WACHACHE ULIMKASIRISHA NYERERE

KATIKA  mazingira ambayo yalijengeka miongoni mwa wavuna jasho  kwamba badala ya kuwatetea wavuja jasho  ni kule kuendelea kwao kujitengenezea mifumo ya kujineemesha na ambayo ilikuwa inajionesha kupitia chama tawala.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliweza kuliona hilo ndani ya CCM aliposema kwa uwazi bila kificho kwamba, CCM kimekuwa chama cha viongozi badala ya kuwa chama cha wanachama.

Jambo hilo ndilo lililompandishia hasira na akasema, “Chama mimi si mama yangu.  Kwangu mimi chama ni sera… chama kile (CCM) kikiziacha shabaha zile na mimi natoka…mimi sio mwenzenu tena.  Leo nawaeleza ukweli tu”.

Kwa bahati mbaya leo hii Mwalimu Nyerere hayupo na imetimia miaka 18 tangu alipoaga dunia la sivyo tungeweza kushuhudia mambo mengi  na huenda yangekuwapo matendo ya woga  katika utekelezaji wa  yale ambayo yamekuwa yakifanyika kinyume na misingi iliyokuwa inawatetea wavuja jasho.

Akitetea utamaduni wa kuhitilafiana, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:  “Msikae hapa mnajidanganya, mnasema sisi tuna utulivu kisiasa… this is nonsense (huu ni upuuzi). Utamaduni wa kuficha matatizo makubwa na kuyafanya kwamba si matatizo ndilo tatizo moja kubwa tulilonalo.”

Hali kadhalika Mwalimu alishangaa kuhusu kuvunjwa kwa Azimio la Arusha ambapo alisema  kuwa miiko iliyokuwa inasimamia maadili ya uongozi ilitupwa na kwa wale waliolikwepa au kulizika na kupata utajiri wa haraka haraka wamezidi kuwa matajiri kuliko hata walivyokuwa kabla.

Hali hiyo inamaanisha kuwa hofu ya kukwapua mali za umma ilitoweka na hivyo kujenga misingi ya kuvuna jasho la wachache ambao walikuwa na ama hawana taarifa kuwa sera zilizokuwa zinawalinda zilishatupwa  na kusahauliwa.

Leo hii ni wananchi wachache na hususani miongoni mwa wavuja jasho ambao watasema haoni ufisadi, rushwa na wizi wa mali za umma. Aidha ni wachache ambao hawatakuwa wanakasirishwa na uzembe wa watendaji wa kuwatumbukiza kwenye lindi la umaskini. Kadhalika ni wachache watakaokuwa hawaoni ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma kupitia Serikali za Mitaa na zabuni mbalimbali.

Lakini kwenye hotuba yake ya Mei 1989, ikiwa ni miaka miwili kabla ya kuzikwa kwa azimio lile aliloliasisi alipokuwa akifungua semina ya wazalishaji wakubwa iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na akiwa alishaona hali itakavyokuwa mbeleni, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Si kwamba Azimio la Arusha limeondoa umaskini hata kidogo, wala halikutoa ahadi hiyo.

“Azimio la Arusha limetoa ahadi ya matumaini. Ya haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio watu wengi wa Tanzania wanaendelea na kuwa na matumaini hayo.

“Madhali yapo matumaini hayo, mtaendelea kuwa na amani … Kama wengi hawana matumaini, tunajenga ‘Volcano’. Siku moja italipuka na lazima ilipuke.

“Isipokuwa watu hao wajinga. Wengi wa nchi hiyo wajinga, wanakubali kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa hivi hivi na wingi wanao, wajinga hao. Kwa hiyo, Watanzania hawa watakuwa wajinga, wapumbavu, kama wataendelea kukubali kuonewa na watu wachache katika nchi yao. Kwa nini?

Alichokuwa akimaanisha Mwalimu ni kwamba nchi huongozwa na kiongozi mwenye maono au dira  ya kitaifa ambaye atakuwa ni kiongozi mwenye kuchukia ufisadi, ujinga, mwenye kupenda maendeleo ya nchi yake, mwenye kuzionea huruma rasilimali adimu za nchi na asiye kuwadi wa utandawazi, mwenye kuchukia nchi inapoacha kufanya mambo ya maendeleo.

Kwa kuwa alikuwa anayaona mambo ya kijinga  yaliyokuwa na maudhi  alikuwa anaona wazi kuwa kiongozi hawezi kupatikana kwa kuangalia urembo wake, utanashati wake tu, ujana wake, ukabila wake, urefu wake, rangi yake, utajiri wake uwe halali au usio halali na mengine mengi.

Ili kuondokana na mambo ya kijinga  alikuwa anaona kuwa kiongozi ni lazima awe ni mtu anayeweza kuangalia  kwa kina hali ya umaskini na mmomonyoko wa mshikamano wa kitaifa  unaoikabili nchi  licha  ya kuwa na utajiri  mkubwa wa maliasili, utulivu na lugha moja.

Wataalamu mbalimbali waligundua mtazamo huo wa Mwalimu ambapo walikuwa  wakibainisha kwamba tatizo la Tanzania si ukosefu wa ajira wala umaskini, bali ni mfumo mbaya wa uchumi ambao haukujali maslahi ya wavuja jasho ambao ndio walio wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles