SERIKALI ya Ujerumani imetangaza kusimamisha mchakato wa kuyashughulikia maombi ya wakimbizi wa Syria wanaotafuta hifadhi. Hatua hiyo imechukuliwa hadi pale tathmini mpya itakapotolewa kuhusu hali ya usalama ya Syria.
Kwa mujibu wa kundi la vyombo vya habari vya nchini Ujerumani, Funke katika ripoti yake, limeinukuu taarifa ya wizara ya usalama wa ndani ikisema maamuzi hayo yamefikiwa hadi mwongozo mpya wa wizara hiyo utakapotolewa hivi karibuni.
Waandishi wa habari wa Funke wamesema kuna hofu kwamba Serikali ya Kansela Angela Merkel itayakataa maombi zaidi ya wakimbizi kutoka Syria iwapo itabainika hakuna machafuko nchini humo.
Kulingana na takwimu za serikali, Wasyria 17,411 walipewa hifadhi mwaka 2018. Baada ya uamuzi wa Merkel wa mwaka 2015 wa kuweka mipaka wazi kwa watu waliokuwa wanakimbia vita, kumekuwa na ongezeko la zaidi ya wakimbizi milioni moja wanaotafuta hifadhi, hasa kutoka Syria, Iraq na Afghanistan.