29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Ujerumani yajitosa Katiba mpya

Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke
Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

UBALOZI wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani nchini umejitosa katika mjadala wa Bunge la Katiba mpya linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.

Pamoja na hali hiyo, Ujerumani imekanusha kuhusika kusaidia kikundi chochote nchini kinachojihusisha na masuala ya siasa, ikiwamo suala la Katiba.

Tamko kwa vyombo vya habari lililotolewa jana na Ofisa Mawasiliano wa Ubalozi wa Ujerumani, John Merikion, limesema Serikali ya Ujerumani kimaadili haiingilii mambo ya siasa za ndani za nchi nyingine.

Tamko hilo limekuja baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agustino Matefu, mwishoni mwa mwezi uliopita kuzituhumu baadhi ya nchi za Ulaya na Asia, ikiwamo Ujerumani kuwa zinafadhili Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukwamisha mchakato wa Katiba mpya.

Matefu, ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la Tanzania Kwanza, nje ya Bunge, alidai kuwa nchi za Uholanzi, Oman na Ujerumani zinahusika na mpango huo kwa kuzitumia taasisi zake za ndani ya nchi.

Kutokana na kauli hiyo, Merikion alisisitiza kuwa Serikali ya Ujerumani na maofisa wake hawafanyi ushawishi wowote kuhusu mwelekeo wa mjadala wa Katiba unaoendelea hivi sasa nchini.

“Kutokana na habari za mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini Tanzania, Ubalozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani unatamka kwamba Serikali ya Ujerumani kimaadili haiingilii mambo ya siasa za ndani za nchi nyingine.

“Kwa hali hii, Serikali ya Ujerumani na maofisa wake hawafanyi ushawishi wowote kuhusu mwelekeo wa mjadala wa Katiba unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania,” ilisema taarifa hiyo ya Ubalozi wa Ujerumani.

Tamko hilo lilizidi kusisitiza kuwa mashirika mengi ya Kijerumani yanafanya kazi na mawakala wa asasi za kiraia duniani kote ili kuimarisha shughuli za mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, aina hiyo ya shughuli za ushirikiano hufanyika pia nchini Tanzania, zikilenga katika mipango ya elimu na mafunzo ambapo utaratibu huo hutolewa kwa wawakilishi wa vyama vyote vikubwa vya siasa nchini.

“Shughuli za kisiasa huwa hazisaidiwi au kufadhiliwa na mashirika haya ambayo hutenda kazi zake kwa kutumia pesa zinazotolewa na Serikali ya Ujerumani,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa ubalozi huo kuzungumzia masuala yanayohusu mchakato wa Katiba mpya unaoendelea nchini.

Tangu Aprili 16, mwaka huu, baada ya Ukawa kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, kumekuwa na madai kadhaa, yakiwamo ya kuwahusisha viongozi wa umoja huo kukwamisha mchakato wa Katiba kutokana na fedha wanazopewa kutoka nchi za Ulaya.

Awali Matefu alidai kuwa taasisi hizo zimekuwa zikifadhili shughuli mbalimbali za Ukawa, ikiwamo kutoa fedha ambazo zimekuwa zikiingizwa katika akaunti binafsi za viongozi wa umoja huo.

Matefu alidai katika kukamilisha mpango huo, Freeman Mbowe na Dk. Willibrod Slaa wamepewa fedha hizo kupitia akaunti zao binafsi kiasi cha Sh 1,700,000 katika awamu ya kwanza, huku awamu ya pili na tatu jumla ikiwa ni dola 850,000.

Mbali na hao, alidai CUF kupitia Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kupitia akaunti yake binafsi amepokea kiasi cha dola za Marekani 400,000 kutoka Oman.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles