SAMWEL MWANGA, MASWA
TATIZO la ajira kwa vijana limekuwa wimbo ambao umeenndelea kuimbwa kila kukicha, huku makundi ya vijana kwa maelfu yakiendelea kurudi mitaani baada ya kumaliza shule na vyuo kila mwaka.
Serikali imekuwa ikiendeela na juhudi zake za kuhakikisha inapata ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana hao, japokuwa aksi ya utatuzi wake imekuwa ikizidiwa kila kukicha.
Mkoani Simiyiu, kama ilivyo katika ameneo mengine nchini, ujenzi wa viwanda katika Wilaya ya Maswa umeendelea kutekelezwa huku kukiwa na matarajio ya kuwanufaisha wananchi kwa kuongeza thamani katika mazao ghafi na kuwezesha kuwepo kwa uhakika wa ajira kwa vijana.
Mbali na kutatua changamoto hiyo kwa wakulima, ujenzi huo wa viwanda pia utasaidia Halmashauri ya wilaya hiyo kutokuwa tegemezi kutokana na mapato kutoka serikalini kwani watakuwa na vyanzo vyao vya mapato ya ndani na hivyo kuwawezesha kufanya shughuli zao walizojipangia za maendeleo kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji mara baada ya kutembelea kiwanda kipya cha kusindika unga wa viazi lishe ambacho kimeshaanza uzalishaji sambamba na kutembelea ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza Chaki na kiwanda cha kutengeneza vifungashio wilayani humo, anasema hiyo ni hatua nzuri kwa Serikali katika kutafuta suluhu ya tatizo la ajira kwa vijana.
Anasema kuwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ulipoingia madarakani chini ya Rais John Magufuli ulijipambanua kuwa ni Serikali ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati na hivyo kutoa maelekezo ya ujenzi wa viwanda katika maeneo yote hapa nchini.
Anasema kuwa awamu hii imepania kuongeza ajira kwa Watanzania kupitia sekta ya viwanda hapa nchini na wilaya hiyo imetekeleza kwa vitendo baada ya kujenga viwanda hivyo vikubwa na kuwa wilaya ya mfano hapa nchini hasa kwa ile miradi ya kimkakati iliyotolewa kwa halmashauri 21 na serikali kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Dk. Kijaji anasema Wilaya ya Maswa wametekeleza agizo la Rais John Magufuli alilolitoa mapema alipoingia madarakani kuwa anataka kuona Tanzania ya Viwanda.
Anasema Maswa wamefanya kwa vitendo kwa ujenzi wa viwanda hivyo vikubwa vitatu cha viazi lishe na vile viwanda vya miradi ya kimkakati cha Kiwanda cha Chaki na kile cha vifungashio mnahitaji pongezi na ndiyo miradi ya mfano hapa nchini kwa zile halmashauri 21 tulizozipatia fedha kwa ajili ya kuitekeleza.
Anasema kuwa ni vizuri sasa viwanda ambavyo havijakamilika ambacho ni kile cha kutengeneza Chaki na kile cha vifungashio vikakamilika kwa wakati na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali inayofikia Sh Bilioni 8 inaonekana na tuhakikishe inatuletea mafanikio.
“Hiyo Shilingi bilioni nane iliyotolewa na serikali thamani yake ionekane kwa ajili ya viwanda hivyo viwili vya miradi ya kimakakati. Hiyo bilioni nane thamani yake ionekane kwa ajili ya viwanda hivyo viwili na ituletee mafanikio ndiyo twende kwenye hiyo sh Bilioni 21 na mnapoaandika maandiko ya miradi ni vizuri yawe yameshiba hivyo tusimame pamoja kusimamia mapato ili tuendelee kuwa na mradi wa kimkakati,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Dk Fredrick Sagamiko anasema kuwa kukamilika kwa viwanda hivyo kutatoa ajira za watu 500 ambao wengi wao watakuwa na vijana.
Anasema kuwa gharama za awali za ujenzi wa viwanda hivyo viwili ilikuwa sh bilioni 8.2 lakini baada ya kuhuisha na kuongeza gharama ya malighafi ambayo ni ya kuchakata chokaa kwa ajili ya utengenezaji wa chaki hivyo gharama ya mradi wote itakuwa Sh bilioni 29.0.
Ni kwa hatua za aina hii, kupitia miradi ya kimkakati na ujenzi wa viwanda vingi, ndipo tatizo la ajira kwa vijana linaweza kupungua na hasa pale ambapo vijana watapewa kipaumbele kwenye kupata ajira ikli waendeshe maisha yao na familia zao