Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amesema mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi utaanza kutekelezwa mwezi ujao ili kumaliza tatizo la mafuriko na uharibifu wa miundombinu unaojitokeza wakati wa mvua.
Mradi huo utatekelezwa kupitia Programu ya Kuendeleza Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 45.
Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Vingunguti, alisema mto huo umekuwa ukizidiwa maji wakati wa mvua na kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
“Tunategemea baada ya mradi huu kuanza kero ya mafuriko itakuwa historia kwa wakazi wa Vingunguti, Mnyamani na Buguruni. Hivyo wananchi muwe na subra,” alisema Mjema.
Awali baadhi ya wakazi wa Kata za Vingunguti, Mnyamani na Buguruni walisema mafuriko yamekuwa kero sugu katika maeneo yao na kuiomba serikali kuufanyia marekebisho Mto Msimbazi.
“Tunataabika sana na mafuriko karibu kila mwaka tunapoteza mali na ndugu zetu kwa sababu ya Mto Msimbazi,” alisema Rashidi Jogaya, mkazi wa Mnyamani.
Katika hatua nyingine DC huyo pia aliagiza kufungwa kwa baa zinazoruhusu watu kucheza wakiwa watupu kwani vitendo hivyo ni kinyume na maadili.
“Wengine wanapiga muziki mpaka asubuhi je, kazi wanafanya saa ngapi? Buguruni imechafuka sana nataka tuisafishe, sitaki niambiwe Buguruni kuna vibaka au ukahaba…ongeeni na watoto wenu, waume zenu waache tabia hizo,” alisema Mjema.
DC huyo pia alikagua ujenzi wa majengo matatu katika Kituo cha Afya Buguruni na kumuagiza mkandarasi kuhakikisha hadi Oktoba 15 mwaka huu yawe yamekamilika.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Emily Lihawa, majengo hayo yanagharimu Sh milioni 632.
Nao baadhi ya wafanyabiashara katika machinjio ya Vingunguti walilalamikia kuporomoka kwa bei ya ngozi hadi kufikia Sh 500 kwa kipande.
“Ngozi tunauza Sh 500 lakini mkoani inauzwa Sh 5,000 tukiuliza tunaambiwa ngozi ya Vingunguti haifai kwenye soko la dunia,” alisema Shabani Hussein.
Kuhusu kero hiyo mkuu huyo wa wilaya aliahidi kukutana na wafanyabishara hao wiki hii kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo na kero zingine.