Na Mwandishi Wetu,
Siku njema huonekana asubuhi na mwanzo wa ngoma ni lelekwani mvumilivu hula mbivu na hivyo ndio hali halisi kwa Tanzania kuwa mambo yameiva kuanza mwendo mrefu wa kufanya nchi hii kuwa kitovu cha biashara ya mafuta na nishati katika eneo hili la Afrika Mashariki.
Kama nchi kibindoni ina hazina ya gesi asilia ya futi za ujazo trilioni 57.2 na imeanza kufanya maunganisho ya wenye rasilimali kwa kujenga bomba la gesi toka Mtwara had Dar na mbioni kujenga lile la Uganda la mafuta ghafi ya nchi hiyo ambapo watu zaidi ya 5000 wataajiriwa kufanya kazi .
Dalili za mvua ni mawingu na hivyo kitendo cha serikali ya Uganda kumilikisha kwa kutoa leseni za uzalishaji mafuta kwa kampuni tatu za Tullow Oil, Total na China National Oil Company (CNOOC) zimefungua ukurasa mpya wa masuala ya mafuta nchini humo na eneo lote la Afrika Mashariki na kuanzisha mbio kamili kuelekea kuzalisha mafuta katika eneo hili.
Leseni nane zilitolewa na Uganda huku ile ya kampuni ya China ilitolewa awali mwaka 2013 kwani ni kati ya serikali na serikali ili Uganda ipate mkopo wa dola milioni 600 za kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa maji kwenye mlango mmojawapo wa mto Nile
Kwa Tanzania kwa hatua hii ya Uganda maana yake ni kuwa ule mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi bandari ya Tanga utafanyika na kielelezo tosha kuwa iwe tayari kwa hilo.
Kabla ya hayo nchi yetu ilitembeleewa na ujumbe wa Ufaransa ikiwa ni ule wa serikali ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na ule wa kamapuni ya Total toka makao makuu kuja kufanya tathmini ya mambo na hali ya mwenendo wa mradi tarajiwa. Dola bilioni 4 sio rasilimali ndogo kwa nchi yeyote ile.
Itakumbukwa mradi huo wa bomba una umbali wa kilometa 1440 na unakisiwa kugharimu zaidi ya dola bilioni 4na hivyo kufanya kuwa ni mradi mkubwa sana wa nishati katika eneo hili.
Kwa maelezo ya Waziri wa Nishati na Mafuta wa Uganda Irene Muloni Uganda ilitoa leseni tano kwa Tullow Oil ambayo ni kampuni iliyosajiliwa Uingereza kama tafutaji mafuta na tatu kwa kampuni ya Total ya Ufaransa wakati CNOOC ya China leseni moja kuanzia mwaka 2013. Mgawo wake ni kuwa Total imepewa leseni Exploration Area One (EA1) na Exploration Area Two (EA2) kwa Tullow Oil na hivyo kurasimisha uwepo wao wa kuchimba mafuta nchini humo na upatakanaji wa mafuta ghafi ambayo yatasafirishwa kupitia bomba linalojengwa na Tanzania kupitia Tanzania.
Habari hizo zilipokelewa kwa shangwe na bashasha na Waziri wa Madini na Nishati wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikaribisha maendeleo hayo na kudiriki kusema kuwa Tanzania sasa itakuwa kitovu cha biashara ya mafuta kwa kule kujitokeza kwa nchi nyingine kutaka nazo kuhusika na ujenzi wa bomba hilo pamoja na kinu chakuchakata mafuta hayo ya Uganda kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki.
Alisema DR Kongo inataka kushiriki ujenzi wa bomba kwa vile nao wanategemea kupitisha mafuta yao kwenye bomba hilo na vilevile wanahitaji gesi asilia toka Tanzania kwa matumizi ya nyumbani na viwanda kadiri uchumi wanchi hiyo unavyokua kutokana na kushamiri kwa Demokrasia baada ya miaka mingi ya mapambano ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Waziri Irene wa Uganda anasema kutolewa kwa leseni hizo kumekamilisha mazungumzo makali na magumu na sasa kilichobaki ni utekelezaji wa makusudio ya kila mmoja ambaye ni mdau wa biashara hiyo; “Na hivyo kuashiria kuanza kwa kazi madhubuti ya mradi wetu” alisema.
Irene alisema ; “Ninategemea utoaji wa leseni hizo utafuatia na mipango kazi ya kuzalisha mafuta Uganda kwani kila kitu kipo mahali pake kama ilivyopangwa na wadau.”
Utatu wa Total, Tullow na CNOOC kwa pamoja wanamiliki maeneo ya mafuta ya Uganda na leseni hizo zinadumu kwa miaka 25 na inaweza kuongezwa tena kwa kipindi cha miaka mitano zaidi.
Lakini mambo bado hayajakamilika vilivyo wakati huu wa majaribu ambapo bei ya mafuta bado ikochini na hivyo kupunguza ari na hamasa ya kuwekeza kwenye sekta hiyo na hivyo basi Tullow na Total wana miezi 18 ya kufanya uamuzi wa mwisho wa kuwekeza baada ya kupata leseni na hivyo kumfanya Waziri Irene aseme kuwa kuzalisha petroli ghafi kibiashara kutafanyika kuanzia mwaka 2020 ikiwa miaka zaidi ya 12 tokea mafuta yagunduliwe.
Wachunguzi wa mambo ya mafuta wanasema kuwa mafuta Uganda yaligunduliwa miaka zaidi ya kumi iliyopita lakini uzalishaji wake umetawaliwa na mbinde kwa kucheleweshwa haswa na serikali kudai kupata donge nono zaidi kutoka kwa wawekezaji kuhusu kodi na mikakati ya uendelezaji wa maeneo hayo. Mwishowe wamefanikiwa kwani watu husema mtafutaji hachoki akichoka amepata!
Wakati uzalishaji utakapoanza Waziri huyo wa Uganda anasema kiasi cha mafuta kitakachopatikana kwa siku kitakuwa ni mapipa 200,000 hadi 230,000.