BRUSSELS, UBELGIJI
MKUU wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya (EU) katika suala la Uingereza kuondoka kutoka umoja huo maarufu kama Brexit, Michel Barnier ameonya Uingereza inaelekea katika hatari ya kuondoka bila makubaliano
Barnier ameyasema hayo mjini hapa jana, siku moja tu baada ya wabunge wa Uingereza kushindwa kuungana ili kupitisha mpango wa kujitoa uliofikiwa na Waziri Mkuu Theresa May mwaka uliopita.
Mjumbe huyo wa majadiliano amesema, EU haina nia ya kutengana na Uingereza bila makubaliano maalumu lakini hawatakuwa na jinsi kutokana na hali ilivyo sasa.
Barnier ameongeza kuwa ingawa mchakato wa Brexit umekuwa mgumu kutekelezeka, Umoja wa Ulaya uko imara.
Kwa mujibu wa Barnier kwakuwa hapakuwa na mtizamo chanya wa walio wengi juu Uingereza kujiondoa kabla ya Machi 29, Kifungu cha 50 kimeongezwa muda hadi Aprili 12.
Barnier ameonya kama May atashindwa kupitisha mpango wake kwa Bunge, basi Uingereza itasalia na njia mbili pekee.
Nazo ni kuondoka bila makubaliano au kuomba upya kuongezewa muda kupitia kifungu cha 50 na kwamba hatua hiyo itapaswa kufanyika kabla ya Aprili 12.