NAIROBI, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta amesema China si nchi pekee inayotoa mikopo kwa nchi yake, na madeni yanayoikabili Kenya hayasumbui.
Alisema hayo hivi karibuni alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Marekani.
Pia alisema Kenya ina mchanganyiko mzuri wa madeni, na kwamba nchi nyingine nyingi zikiwemo Japan na Marekani pia zimewapa mikopo.
Alidokeza kuwa Japan ni upande unaotoa mikopo mingi zaidi kwa mradi wa bandari ya Kenya, na Ufaransa ni mfadhili mkuu wa miradi ya uzalishaji umeme.
Akijibu wasiwasi kuhusu mikopo kutoka China kusababisha msukosuko wa madeni nchini Kenya, Rais Uhuru alisema; “Tunakopa fedha kutoka China, pia Marekani.
“Tunatakiwa kuziba pengo la ujenzi wa miundombinu, tutashirikiana na washirika duniani kote wanaopenda kushirikiana nasi na kutusaidia kutimiza ajenda za kijamii na kiuchumi.
“Hivyo, kwanini tumfuatilie mfadhili mmoja tu? Ukweli ni kwamba kwangu mimi hali ya madeni yetu ni ya pande nyingi, kwa mfano Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
“Kama nilivyosema, Japan, China na Ufaransa zinashirikiana nasi na kutusaidia kutimiza malengo.”