NA AZIZA MASOUD,
SABABU  mbalimbali za kijamii,kimahusiano na kifamilia zinawafanya watu  wanaokuwa wameshapata mtoto ama watoto  wanashindwa kuishi pamoja kabla au  baada ya ndoa.
Masmbo hayo husababisha watu kutengana vyumba maana wanakuwa wanaonekana wanatoka nyumba moja lakini wanaishi  vyumba tofauti.
Wengine wanakuwa wanaishi chumba kimoja lakini vitanda tofauti ama wanalala kitanda kimoja hawaongei.
Pia wapo ambao wanafikia hatua mbaya zaidi ya kila mtu kuishi mahala pake hii si nzuri kwa ustawi wa mtoto.
Katika mazingira hayo wahusika wasipokuwa makini  hasa mzazi mmoja anapoamua kuishi na mtoto anaweza akawa sehemu ya kumtengeneza mtoto kumchukia mzazi mwingine.
Mara nyingi hali hiyo huchangiwa na ubinafsi wa mzazi unaochangiwa  na hasira ama visasi vya upande wa pili na kudhani kuwa akimtengenezea mtoto chuki baina ya mzazi mwenzie itakuwa kama njia ya kumkomoa.
Hii si nzuri wazazi mnapaswa kuwa waangalifu katika hili,si vizuri ugomvi wenu kumuingiza mtoto mtachangia kumuharibu kisaikolojia.
Wapo watoto ambao wanachelewa kupata ufahamu lakini hivyo ugomvi huo hautamsumbua lakini baadhi huwai kupata ufahamu wa kiakili hivyo masuala ya namna hiyo yanakuwa yanamfanya anashindwa kufanya mambo ya msingi na kuwa sehemu ya mgogoro wa wazazi.
Wengine wanafikia hatua ya kushindwa kuhudhulia masomo yao vizuri na kupata matokeo mabaya katika mitihani kwa sababu tu kufikiria maisha wanayoishi wazazi wake.
Mnapojenga chuki si kwamba mtaendelea kuwa maadui kwakuwa kikawaida wazazi mara nyingi huwa wanasameheana lakini mtoto bado anakuwa na kinyongo kiasi cha kufikia hatua ya kushindwa kumpa msaada wa anapokuwa na uwezo mzazi husika na kufanya kama sehemu ya kulipiza kisasi.
Hiyo inachangiwa na mzazi ambaye alikuwa akimlea mtoto huyo  na kutumia muda mwingi kumsema vibaya mzazi mwenzie.
Kumpandikiza chuki mtoto akiwa mdogo kuna athari kubwa anapofikia umri wa utu uzima,.
Ili kumjengea mazingira mazuri kila mzazi anatakiwa atekeleze majukumu yake ya kimalezi kama ni baba hakikisha unatoa fedha za matumizi na mambo mengine ya msingi kwa wakati.
Mnapoishi tofauti ama mnatakiwa kushirikiana katika malezi ili mtoto aweze kupata malezi bora.
Mzazi anayelea mtoto peke yake bila msaada wa mwenzie anapaswa  kuwa makini,hata kama mmegombana mtoto hapaswi kufahamu matatizo yenu ili kumjengea ustawi mzuri katika makuzi.