27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAENDELEO YETU YANADUMAZWA KWA KUCHEKELEA TOFAUTI ZETU

Baadhi ya Viongozi waliounda Ukawa
Baadhi ya Viongozi waliounda Ukawa

Na MARKUS MPANGALA,

KIWANGO cha mgawanyiko katika Taifa letu kimekuwa kikubwa. Mgawanyiko mkubwa umejengwa katika maeneo makuu manne; kwanza kuna wale wanaojitenga au kujiengua kwa misingi ya itikadi za vyama vya siasa.

Kundi hili limekuwa likijiona kuwa wao ni ndugu, marafiki na watu wanaoaminiana zaidi kuliko kundi lolote. Watu wa kundi hili wamekuwa na kasumba kwamba mtu yeyote mwenye mawazo tofauti na wao ni mpinzani wao.

Kundi hili hutawaliwa na kambi kuu mbili; wafuasi wa vyama vya upinzani ambavyo vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi-Ukawa na wafuasi wa Chama tawala CCM. Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NLP na NCCR-Mageuzi.

Makundi mawili hayo yametawala mno siasa za vijana maeneo mbalimbali. Vijana wa kike na kiume, wazee wetu wanaume na wanawake, watu wa makamo nao wamekuwa wakijigamba kuwa kwenye kundi lao halipokei wale wenye fikra za katikati au kutofungamana na upande wowote.

Kiwango cha kurushiana mashambulizi ya maneno kwenye mitandao ya kijamii ni ishara tosha kuwa makundi haya hayawezi kuketi pamoja na kunywa kahawa wala juisi.

Kumekuwa na mparaganyiko ambao umejenga dhana kuwa watu wa makundi hayo hawapaswi kupiga soga la aina yoyote na wale wa kundi jingine. Kifupi kuna ufa katikati ya pande hizo mbili.

Kundi la tatu ni wale ambao wamejipambanua kutofungamana na upande wowote lakini hawaaminiki kokote. Katika kundi hilo kimeibuka Chama cha ACT-Wazalendo ambacho hakina mfungamano na Ukawa wala chama tawala.

Kundi la wasiofungamana na upande wowote hutumia mantiki kuamua mambo. Ni kundi ambalo mantiki inaongoza au ni msingi wa kujadili hoja zao dhidi ya makundi yote mawili.

Pengine hayo ni matunda ya kile tunachokisema; ufuasi wa watu unapozidi itikadi. Kumekuwa na kasumba ya kuchagua upande na hilo si jambo baya.

Matunda ya kuchagua upande ni kwamba wale wasio na upande huvishwa kuwa watu wanaotafuta vyeo, miliki au namna nyingine yoyote ya kujikwamua kiuchumi.

Si ajabu kusikia kundi la wana Ukawa wakisema fulani anatafuta ukuu wa wilaya au cheo katika mamlaka fulani ya uteuzi au kundi la CCM kuwashutumu wasio na upande kutumika kukichafua chama chao.

Malumbano ya makundi hayo mawili husababisha fikra za wengine kutawaliwa na jazba mno. Matunda ya malumbano hayo husababisha ufa ambao unatuletea mgawanyiko na kushindwa kushikamana hata kwenye mambo yasiyohusu siasa.

Ni katika muktadha huo, tunajikuta tunajenga kizazi cha watu wanaojitazama kama kundi fulani lenye umoja na jingine ni adui.

Ndiyo kusema kumekuwa na desturi kuwa ili uaminike kwenye kundi lolote, lazima uyatupilie mbali makundi mengine.

Bila shaka hilo ni gereza ambalo linasababisha baadhi ya wafuasi wake kuishia jela kwa kusababisha matusi ama udhalilishaji kwa wengine.

Haigombi kuwa sehemu ya makundi hayo. Lakini hasara ni pale makundi hayo yanapotumika kama nyenzo ya kuangamiza ufanisi wa wengine ama kuchochea ghadhabu na kuudhi badala ya kushindana kuwaletea mambo mema wananchi wake.

Makundi hayo kwa namna fulani hayajadili kuhusu maendeleo, badala yake yanajikita kuangalia nani amesema nini dhidi yao ili waanze kuhamasishana kumshughulikia, kumdhalilisha ama kwa namna nyingine yoyote kuridhisha nafsi zao.

Baadhi yao wamejikuta wakitupwa jela sababu ya kutusi wapinzani wao ama wapinzani kujikuta wakionewa ama kunyanyaswa sababu za upinzani wao.

Jamii inayopendelea kutafuta matatizo ili kuyaendeleza na kuyafurahia, haina muda wa kujadiliana juu ya maendeleo. Jamii ya namna hiyo inajenga kizazi cha vijana wenye kutamani kuongelea migogoro na mizozo isiyo na kichwa wala miguu.

Ndiyo kusema ukweli utabaki kuwa ukweli kwamba makutano ya fikra yakinifu ndio uzao wa mambo mapya. Ifike wakati tujifunze kuweka misingi mizuri ya taifa hili kwa masilahi ya kesho.

Siasa ni sehemu ndogo sana katika taifa hili kuliko hata nchi yenyewe, viongozi wanapaswa kutafakari kwa kina umuhimu wa taifa hili la Tanzania kwa Watanzania.

Wapo wanaodiriki kujaribu kupindisha ukweli kwa masilahi ya kisiasa, tutambue kwamba siasa zitapita lakini Tanzania yetu itabaki, hivyo ni vema kutengeneza misingi bora ya kulikuza taifa hili na si misingi ya kunufaisha watu wachache kwa manufaa ya vyama vyao au itikadi zao.

Hakuna maendeleo yanayopatikana kwa kutumia nguvu nyingi kusaka matatizo na migogoro ili tupoteze muda kutatua na kusuluhisha.

Itikadi nzuri ya chama kwa wafuasi wake ni ile inayohakikisha inaheshimu nafasi ya watu wengine wakiwamo wapinzani wao au watu wasiofungamana na upande wowote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles